Kamati simamizi ya chama tawala cha Jubilee imependekeza kung’olewa kwa naibu rais William Ruto kama naibu kiongozi wa chama hicho.
Katibu mkuu wa chama hicho Raphael Tuju anasema Ruto aliacha kuwa naibu kiongozi wa chama hicho aliporuhusu kufunguliwa kwa chama kingine cha Jubilee Asili.
Na huku baraza kuu la chama hicho likitazamiwa kuamua hatma ya uamuzi huo, Tuju amesema Ruto hakaribishwi katika makao makuu ya Jubilee, Pangani kwa sababu anatumia afisi hizo kuendeleza azma yake ya kumrithi rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Katibu huyo mkuu aidha amemkosoa Ruto kwa kukosa kuhudhuria kongamano la hivi punde lililoandaliwa kuangazia hatua zilizopigwa katika vita dhidi ya corona.
Haya yanajiri siku moja baada ya Ruto akiwa ameandamana wabunge zaidi ya thelathini wa chama hicho kukutana katika makao makuu ya chama hicho kujadili maswala mbalimbali ikiwemo ushauri wa kulivunja bunge.









