Chuo Kikuu cha Mafunzo ya Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kimeiambia Shirikisho la Watumiaji Bidhaa Nchini (COFEK) kwamba mbunge wa Kimilili Didmus Barasa hakuwa mwanafunzi katika taasisi hiyo ya masomo ya juu.
Chuo hicho kikuu kimekanusha kumtuza Barasa shahada ya uhandisi wa umeme mnamo Mei mwaka 2008.
Katika barua iliyoandikwa tarehe 14 Septemba, 2026 msajili wa chuo hicho Dr. Aggrey Wanyama alisema kuwa jina la mbunge huyo halikuonekana popote kwenye rekodi zao.
Zaidi, JKUAT ilipinga uhalali wa shahada ya mbunge huyo ikisema kwamba haikuwa na sherehe yoyote ya kufuzu mwezi Mei mwaka 2008.
Kutokana na hilo, chuo hicho kikuu kilifikia uamuzi kuwa cheti hicho cha shahada ya uhandisi wa umeme ambacho mbunge huyo aliwasilisha hakikuwa halali.
‘‘Jina lake halipatikani katika rekodi zetu za wanafunzi wa awali, na JKUAT haikuwa na sherehe zozote za kufuzu mwezi Mei 2008. Kwa hivyo cheti chake cha shahada ya Programu ya Uhandisi wa Umeme si halali.’’ Alisema Dr Aggrey Wanyama, msajili wa chuo hicho.
Zaidi JKUAT iliongeza kuwa suala hilo lilikuwa awali limeibuliwa na tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC), ambayo ilipewa taarifa kuhusu uhalali wa kuhitimu kwa masomo.
‘‘Suala hili lilikuwa awali limechunguzwa na tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC) pamoja na bodi ya wahandisi nchini (EBK), na taarifa sawia iliwasilishwa kwa mashirika hayo yote.’’ Msajili alisema.
Hili linajiri baada ya COFEK kuelekea mahakamani kutaka udhibitisho wa viwango vya masomo ya mbunge huyo alipoweka wazi kuwa angekuwa akifuzu na shahada ya uzamifu ambayo alituzwa mwezi Agosti 2026 kutoka chuo kikuu cha Murang’a.









