Mahakama yampata Kanja na hatia

0
Inspekta jenerali wa polisi Douglas Kanja katika kikao na wanahabari (awali)

Mahakama Kuu imempata Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na hatia ya kuidharau mahakama, kufuatia kushindwa kwa polisi kutekeleza amri iliyowataka kutoa notisi kwa umma mapema kabla ya kuweka vizuizi barabarani.

Jaji Patricia Nyaundi amesema Kanja alishindwa kuhakikisha kwamba maafisa wa polisi wanazingatia amri za muda zilizotolewa na Jaji Lawrence Mugambi tarehe tisa Julai, 2025.

Kutokana na uamuzi huo wa Alhamisi tarehe 17 Septemba 2026, Kanja ameagizwa kufika mbele ya Mahakama Kuu tarehe 28 Septemba, 2026, kwa ajili ya kusikilizwa na kisha kutolewa kwa hukumu.

Kesi hiyo ilitokana na hatua ya polisi kuweka vizuizi kwenye barabara kuu zinazoelekea Katikati mwa jiji kuu la Nairobi wakati wa shughuli za kuadhimisha maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa mwaka 2024.

Katiba Institute, ilipinga hatua hiyo ya polisi, ikisema vizuizi hivyo viliwekwa bila notisi ya mapema kwa umma kama ilivyoagizwa na amri iliyopo ya mahakama hatua iliyoathiri madereva, wafanyakazi na umma kwa ujumla pamoja na upatikanaji wa huduma muhimu.

Katika uamuzi wake, Jaji Nyaundi amesema suala hilo halikuhusu maandamano pekee na haki ya kikatiba ya kukusanyika kwa amani chini ya Kifungu cha 37 cha Katiba.

Jaji huyo pia alihusisha kesi hiyo na uhuru wa watu wa kutembea na kusafiri unaolindwa chini ya Kifungu cha 39, pamoja na wajibu wa polisi chini ya vifungu vya 10 na 244 kuheshimu utawala wa sheria, haki za binadamu, uwazi na uwajibikaji.

Mahakama pia ilisema Kanja bado ana jukumu la kuhakikisha maafisa walio chini ya uongozi wake wanazingatia amri za mahakama.

Mkurugenzi Mkuu wa Katiba Institute, Nora Mbagathi, amepongeza uamuzi huo, huku akiibua wasiwasi kuhusu kile alichokitaja kuwa ongezeko la matumizi ya kesi za kuidharau mahakama ili kuzilazimisha taasisi za serikali kutekeleza maamuzi ya mahakama.

‘‘Ingawa uamuzi huo unakaribishwa, haja inayoongezeka ya kutumia maombi ya kuidharau mahakama ili kuhakikisha serikali inatii maamuzi ya mahakama haiendani na nchi inayopaswa kuongozwa kwa misingi ya utawala wa sheria na ufuasi wa Katiba.’’ Mbagathi alisema.

Taasisi hiyo ya kutetea haki za binadamu ilikuwa awali imewasilisha kesi mahakamani ikitaka Kanja awajibishwe binafsi kwa madai ya kukiuka amri za mahakama.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here