Mahakama yaamua jinsi ya kujumlisha kura za rais

0

Mahakama Kuu imedumisha mchakato wa kujumlisha na kuthibitisha katika kituo cha kitaifa matokeo ya uchaguzi wa urais, na kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa na seneta wa Busia, Okiya Omtatah, kupinga mchakato huo.

Katika uamuzi wake wa Juma nne tarehe 22 Septemba 2025, mahakama imeunga mkono kifungu cha 39(1C) cha sheria ya uchaguzi pamoja na kanuni ya 83(2) ya kanuni za uchaguzi, ambazo zinaweka utaratibu wa kujumlisha na kuthibitisha matokeo ya urais katika ngazi ya kitaifa.

Katika kesi hiyo, Omtatah alipinga kuanzishwa na uendeshaji wa kituo cha kitaifa cha kujumlisha matokeo, akisema katiba inaipa maafisa wasimamizi wa uchaguzi wa maeneo bunge jukumu la msingi na la mwisho la kujumlisha, kuthibitisha na kutangaza matokeo ya urais.

Pia aliiomba mahakama iamuru Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) izuiwe kujumlisha tena au kuthibitisha upya matokeo ya urais baada ya kutangazwa katika ngazi ya maeneo bunge.

Hata hivyo, mahakama ilibaini kuwa kujumlisha matokeo katika ngazi ya kitaifa ni muhimu ili kubaini iwapo mgombea wa urais ametimiza kiwango cha kikatiba kinachohitajika ili kushinda uchaguzi.

Kwa mujibu wa katiba, mgombea wa urais lazima apate zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa, pamoja na angalau asilimia 25 ya kura zilizopigwa katika zaidi ya nusu ya kaunti nchini.

Katika uamuzi wake, jaji Gregory Mutai alisema kiwango hicho cha masharti mawili kinaweza kubainishwa pekee kupitia kujumlisha matokeo ya urais katika ngazi ya kitaifa.

“Kwa hivyo, zoezi la kujumlisha na kuthibitisha matokeo kitaifa si mzigo wa ziada unaowekwa kwa wagombea wa urais au wapiga kura.”

Huku ikiunga mkono kujumlisha matokeo kitaifa, mahakama ilifafanua kuwa mchakato huo hauipi IEBC mamlaka ya kubadilisha matokeo yaliyotangazwa katika vituo vya kupigia kura.

Ilisisitiza kwamba iwapo kutakuwa na tofauti kati ya matokeo yaliyotumwa kielektroniki na matokeo halisi kutoka kituo cha kupigia kura, matokeo yaliyothibitishwa na kutangazwa katika kituo hicho ndiyo yatakayotambuliwa.

Mahakama pia ililitaka bunge kupitia upya sheria za uchaguzi nchini kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ikisema kwamba wabunge wanapaswa kuandaa sheria za uchaguzi bila kujua ni wanasiasa au maslahi gani hatimaye yatanufaika kutokana na sheria hizo.

Kwa mujibu wa mahakama, mtazamo huo utasaidia kuandaa sheria za uchaguzi zinazolinda maslahi mapana ya wakenya badala ya “malengo finyu, ya muda na yanayobadilika” ya wanasiasa.

Uamuzi huo unajiri wakati Kenya ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu, huku masuala ya kujumlisha, kuthibitisha na kutangaza matokeo ya urais yakitarajiwa kuendelea kuwa sehemu muhimu ya mageuzi ya uchaguzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here