Uhuru ampokeza Matiang’i usukani wa Jubilee

0

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta amemkabidhi naibu wake, Fred Matiang’i, uongozi wa chama cha Jubilee.

Hata hivyo, Uhuru amesema ataendelea kuwa mwanachama, akikanusha mipango ya kujiondoa kabisa katika chama hicho kinapojiandaa kwa siasa za uchaguzi mkuu wa 2027.

“Tunaposubiri NDC, nimeamua kumwachia naibu wangu aongoze chama. Ningependa kuwaomba kwa heshima mumkubali Fred Matiang’i achukue nafasi ya kiongozi wa Jubilee Party,” Uhuru alisema.

Uhuru amesema anaichukulia Jubilee kama makao yake ya kisiasa na anataka kuendelea kushiriki katika shughuli za chama hicho hata baada ya kuachia nafasi yake ya sasa ya uongozi.

Akizungumza Juma nne tarehe 22 Septemba 2026 wakati wa makabidhiano ya uongozi wa chama, Uhuru alisema anapanga kuchukua nafasi ya mshauri mkuu ndani ya chama, ambapo ataendelea kuwaunga mkono viongozi wake na kutoa ushauri kuhusu masuala ya kisiasa.

“Siwezi kuiacha Jubilee Party; nikiiacha chama niende wapi? Nina nyumba nyingine? Si hii ndiyo tuliyojenga pamoja? Nataka kuchukua nafasi ya juu na kuwa mshauri mkuu. Watu wakija na wanataka kuniona, bado nitakuwa hapa, lakini kunapokuwa na mkutano, nitakuwa nimekaa mahali pamoja nanyi,” Uhuru alisema.

Maendeleo hayo yanajiri wakati Jubilee inaanza maandalizi ya mabadiliko ya uongozi kufuatia uamuzi wa mahakama kuu uliowazuia marais wastaafu kushikilia nyadhifa za uongozi katika vyama vya kisiasa zaidi ya miezi sita baada ya kuondoka madarakani.

Rais huyo wa nne wa Kenya alikosoa serikali tawala chini ya mrithi wake rais William Ruto kwa kuendelea kumlaumu miaka minne baada ya kuingia madarakani, akiitaka itekeleze wajibu wa kuwatumikia wakenya.

“Mahakama iliposema wameshinda, mlituona tukipigana? Tuliwapa vyombo vyote vya mamlaka mchana kweupe. Haikuwa usiku; hakukuwa na vita,” Uhuru alisema.

“Na baada ya miaka minne, bado anasema Uhuru hivi, Uhuru vile. Ulipewa uongozi ili uendelee kuzungumzia Uhuru? Au ulipewa uongozi ili kuwatumikia wakenya?”

Uhuru alisema viongozi mara nyingi hutafuta mtu wa kumlaumu mambo yanapokwenda tofauti na ilivyotarajiwa, lakini akaonya kuwa wakenya wanaweza kutofautisha kati ya maelezo yanayotolewa na hali halisi wanayopitia.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here