Uchungu wa mwana; mama aliyejifungua watoto watano kwa mpigo awapoteza

0

Furaha ya Mercy Kanini ya kujifungua watoto watano kwa wakati mmoja imegeuka na kuwa huzuni kubwa kufuatia kifo cha mtoto wa tano na wa mwisho aliyekuwa bado hai katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

KNH ilitangaza Jumatano tarehe 16 Septemba kwamba watoto wote watano wachanga, ambao walikuwa wamehamishwa kutoka Hospitali ya Thika Level Five kaunti ya Kiambu kwa ajili ya kupata huduma maalumu za matibabu kwa watoto wachanga, walikuwa wamefariki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu afisa mkuu mtendaji wa KNH, Dkt. Joel Lessan, watoto hao walizaliwa kabla ya wakati wao, wakiwa na takribani wiki 25 za uja uzito, na walikuwa na uzito wa chini sana na uliokuwa hatarishi wakati wa kuzaliwa.

“Licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na timu zetu za matibabu na huduma maalumu walizopewa, kwa masikitiko makubwa watoto wote watano walifariki,” alisema Lessan.

Hospitali hiyo ilisema timu yake ya wataalamu mbalimbali wa kitengo cha watoto wachanga, iliyojumuisha madaktari bingwa wa watoto wachanga, wauguzi na wataalamu wengine wa afya, ilitoa huduma maalumu na kufanya kila juhudi kuwasaidia malaika hao.

KNH ilieleza kuhuzunishwa sana na vifo hivyo na kutoa pole kwa familia, ikisema inatambua maumivu makubwa yanayotokana na kupoteza watoto watano wachanga.

Vifo hivyo vilitokea siku mbili baada ya watoto hao kuhamishiwa KNH kufuatia kuzaliwa katika Hospitali ya Thika Level Five mnamo Septemba 13.

Watoto hao, wasichana wanne na mvulana mmoja, walizaliwa kwa njia ya kawaida na Kanini mwenye umri wa miaka 28, mkazi wa Juja katika Kaunti ya Kiambu.

Kuzaliwa kwao kulikuwa kumeiletea familia ya Kanini furaha kubwa hapo awali baada yake kujifungua watoto wote kwa njia ya kawaida, katika tukio ambalo lilielezwa kuwa ni la nadra yakiwa matukio matano pekee ya aina hiyo yaliyokuwa yamewahi kurekodiwa nchini.

Watoto hao walikuwa sehemu ya uzao wa tatu wa Kanini ambaye tayari alikuwa na mtoto wa kiume na mtoto wa kike, mumewe, Evans Nyamhanga, akielezea kama muujiza na kwamba familia ilikuwa ikitarajia kupata watoto wanne.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here