Serikali Yaahidi Usalama Kuelekea Uchaguzi Wa 2027.

0
Waziri mwenye mamlaka Makuu Musalia Mudavadi Katika Kongamano la Kwanza wa Robo Mwaka la Kidiplomasia la 2026, Jijini Nairobi
Waziri mwenye mamlaka Makuu Musalia Mudavadi Katika Kongamano la Kwanza wa Robo Mwaka la Kidiplomasia la 2026, Jijini Nairobi

Serikali itaongeza hatua za usalama na ushirikiano kati ya idara mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027, ili kubaini na kukabiliana na vitisho vinavyojitokeza kabla ya siku ya kupiga kura.

Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi amesema serikali itahakikisha usalama wa Wakenya, taasisi za uchaguzi na miundombinu muhimu katika kipindi chote cha uchaguzi.

Akizungumza wakati wa Mkutano wa Kwanza wa Robo Mwaka wa Kidiplomasia wa 2026, Jijini Nairobi Mudavadi amesema watu watakaotishia amani na usalama watawajibishwa kwa mujibu wa sheria, bila kujali misimamo yao ya kisiasa au hadhi yao.

Amesema usalama wa taifa, amani na utulivu wa nchi ni kipaumbele kikuu cha serikali kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Mudavadi pia ametaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, kuruhusiwa kutekeleza majukumu yake ya kikatiba kwa uhuru huku akionya dhidi ya juhudi za kuidhalilisha tume hiyo.

Amewataka wadau wote kuheshimu na kuimarisha taasisi za kikatiba, akisema demokrasia inategemea taasisi imara na kuheshimiwa kwa sheria zilizowekwa.

“Sote tuna jukumu la kuheshimu na kuimarisha taasisi zetu za kikatiba. Demokrasia hudumishwa na taasisi imara na kuheshimiwa kwa sheria zilizowekwa, wala si maslahi ya mtu binafsi,” amesema Mudavadi.

Aidha amesema serikali imejitolea kuhakikisha uchaguzi wa 2027 unakuwa salama, huru na wa amani kupitia mipango kama vile Mchakato wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano, NCIC, ya kukomesha ghasia wakati wa uchaguzi wa 2027, inayojulikana kama Uchaguzi Bila Noma.

Mudavadi, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje amezitaka balozi zinazopanga kutuma waangalizi wa uchaguzi nchini kuanza maandalizi mapema na kutimiza masharti ya IEBC ili kupata vibali kwa wakati.

“Kwa wale wanaopanga kuleta waangalizi wa uchaguzi, tunawahimiza kuanza maandalizi mapema ili kuhakikisha wanapata vibali kwa wakati na kuepusha usumbufu unaoweza kutokana na kutotimiza masharti,” amesema Mudavadi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here