
Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi amesema Kenya haijaweka marufuku ya jumla kwa raia wa kigeni wanaojihusisha na biashara ndogo nchini, akisema serikali inalenga kuhakikisha shughuli zao zinafanyika kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa Kwanza wa Robo Mwaka wa Kidiplomasia wa 2026, Jijini Nairobi Mudavadi amesema agizo la hivi karibuni kuhusu wafanyabiashara wa kigeni linalenga kuhakikisha wanazingatia Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na sheria za Kenya vilevile kulinda riziki za Wakenya
“Kenya haijaweka marufuku ya jumla kwa raia wa kigeni wanaojihusisha na biashara ndogo. Hatua zinazochukuliwa ni za udhibiti na si za kibaguzi,” amesema Mudavadi.
Mudavadi, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, amesema Kenya bado iko wazi kwa biashara ndogo na kubwa za raia wa kigeni wanaotimiza masharti ya uhamiaji, vibali vya kazi, usajili wa biashara na leseni.
Amewataka raia wa nchi wanachama wa EAC wanaofanya biashara nchini kuheshimu sheria zinazohusu kuingia, kukaa na kutoa huduma nchini.
“Raia wa nchi wanachama wa EAC wanapaswa kuheshimu sheria za nchi zinazowasimamia kuhusu kuingia, kukaa na kutoa huduma ndani ya mamlaka ya Kenya,” ameongeza Mudavadi.
Wakati uo huo amesisitiza kuwa yeyote anayewatishia raia wa kigeni au biashara zao atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Amesema Kenya bado imejitolea kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kutekeleza Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063, ikiwemo kuwezesha uhuru wa watu, mitaji, bidhaa na huduma za kusafiri.
Ufafanuzi huo umetolewa baada ya Rais William Ruto kuielekeza serikali kuchukua hatua kuhusu ushiriki wa raia wa kigeni katika biashara ndogo ndogo nchini.








