Oburu apokea mikoba ya IPOA

0

Duncan Ojwang Oburu ameapishwa kuwa mwenyekiti wa nne wa Mamlaka Huru ya Kutadhmini Utendakazi wa Polisi (IPOA).

Ojwang ameapishwa katika hafla iliyoongozwa na Jaji Mkuu na rais wa mahakama ya upeo, Martha Koome, ikifanyika katika Mahakama hiyo, ambapo Msajili Mkuu wa mahakama, Winfridah Mokaya, alisimamia kiapo chake cha kuingia madarakani Alhamisi tarehe 10 Septemba.

Jaji Mkuu Koome alimtaka mwenyekiti huyo mpya wa IPOA kutekeleza majukumu yake kwa uhuru, ujasiri na kutokuwa na upendeleo.

“Ninakuhimiza kuchukua jukumu hili kwa unyenyekevu, ujasiri na kujitolea bila kuyumba kwa kuzingatia katiba,” alisema Koome.

Alimtaka Ojwang kuhakikisha kuwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) inafanya kazi kwa weledi, kwa mujibu wa sheria na kwa kuheshimu utu na haki za Wakenya.

“Iongoze IPOA kwa uhuru. Iongoze kwa ujasiri na haki. Lazima uwe thabiti, usiwe na upendeleo na utegemee ushahidi, huku ukiheshimu taratibu zinazotakiwa kisheria,” alisema.

Ojwang anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Jaji Ahmed Issack Hassan, ambaye aliacha wadhifa wa mwenyekiti wa IPOA mwezi Februari 2026 baada ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa.

Naibu Mwenyekiti wa IPOA, Ann Wanjiku Mwangi, baadaye alihudumu kama mwenyekiti wa kikaimu wakati mchakato wa kumpata mrithi ulipoanza.

Mchakato wa kuajiri ulianza Julai 2026 baada ya rais William Ruto kuunda jopo la kutambua, kuwahoji na kupendekeza wagombea wanaofaa.

Baadaye Ojwang aliteuliwa na rais na kuhojiwa na Bunge la Kitaifa ambalo liliidhinisha ripoti husika ya kamati tarehe 19 Agosti, na hivyo kuwezesha uteuzi wake ambao ulichapishwa rasmi katika Gazeti la Serikali tarehe 31 Agosti 2026.

IPOA imepewa jukumu la kutoa usimamizi wa kiraia wa NPS, kuchunguza malalamiko na vifo vinavyotokana na vitendo vya polisi, pamoja na kukuza uwajibikaji ndani ya Huduma hiyo.

Katika hotuba yake baada ya kuingia rasmi ofisini, Ojwang aliahidi kulinda uhuru wa mamlaka hiyo akipokelewa na naibu mwenyekiti, Mwangi aliyeeleza Imani kuwa uzoefu na ujuzi wake utaimarisha kazi ya taasisi hiyo.

“Tuna imani kwamba uzoefu, ujuzi na mtazamo wako utaongeza thamani kwa IPOA na kwa wananchi wa Kenya,” alisema.

Ojwang ana Shahada ya Uzamifu (PhD) katika Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Arizona, Shahada ya Uzamili ya Sheria katika Haki za Kibinadamu na Sheria ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Indiana pamoja na shahada ya ‘Juris Doctor’ kutoka Chuo Kikuu cha Southern Illinois nchini Marekani.

Pia amewahi kuhudumu katika taaluma ya ualimu wa vyuo vikuu, ikiwemo kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi na kuwa Mkuu wa Kitivo pamoja na Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Africa Nazarene.

Mbali na taaluma ya ualimu, Dkt. Ojwang amehusika katika masuala ya sera za umma na michakato ya utawala.

Alikuwa miongoni mwa watu waliotoa usaidizi wa kitaalamu wakati wa mchakato wa Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo, na pia amehusishwa na kazi za kisera katika sekta ya umma na masuala ya sheria.

Muda wa miaka sita wa Ojwang sasa umeanza huku kukiwa na matarajio kwamba ataongeza uwajibikaji wa polisi, kuboresha namna malalamiko yanavyoshughulikiwa na kuimarisha imani ya umma katika usimamizi wa kiraia wa shughuli za polisi.

Pamoja na Ojwang makamishna wapya wa tume mbalimbali nchini vilevile wameapishwa ili kuanza kutekeleza majukumu yao ya kikatiba.

Wanajumuisha Wilson Sossion na Antonina Lentoijoni wanaojiunga na Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) sawa na Flora Nduku Mutua anayejiunga na tume ya utumishi wa umma (PSC).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here