Gavana wa Migori Zachary Okoth Obado pamoja na wanawe wanne wanatazamiwa kushtakiwa Alhamisi baada ya kukamatwa kuhusiana na sakata ya ufujaji wa Sh73M.
Taarifa kutoka kwa afisa mkuu mtendaji wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC Twalib Mbarak imesema kuwa Obado na familia yake wanatazamiwa kushtakiwa katika mahakama ya hakimu baada ya kusafirishwa hadi Nairobi.
Watoto wa gavana huyo wanaohusishwa na sakata hiyo ni Dan Okoth, Susan Okoth, Jerry Okoth na Adhiambo Okoth.
EACC inasema washukiwa watashtakiwa kwa mashtaka manne ikiwemo kushirikiana kutekeleza ufisadi, ulanguzi wa pesa pamoja na unyakuzi wa mali ya umma
Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Hajji anasema watoto wa Gavana huyo walitumia Sh38M kulipia karo ya shule na matumizi mengine ya kibinafsi wakiwa nchini Australia, Scotland na Uingereza kando na kunua gari aina ya Toyota V8.
Sh34M pia zinadaiwa kutumika katika ununuzi wa nyumba ya kifahari mtaani Loresho Ridge, Nairobi mmiliki wake akiwa ni bintiye gavana Obado, Evelyn Adhiambo Zachary.