Chama cha Jubilee hakitashiriki katika chaguzi ndogo za Machakos, Matungu na Kabuchai

0

Chama tawala cha Jubilee kimesema hakitakuwa na mgombea katika kiti cha useneta kaunti ya Machakos pamoja na maeneo bunge ya Kabuchai na Matungu kaunti ya Kakamega.

Katibu mkuu wa chama hicho Raphael Tuju akihutubia wanahabari amesema sababu kuu ya kutoshiriki katika chaguzi hizo ndogo ni kutokana na ushirikiano wa kisiasa uliopo baina ya vyama mbalimbali ikiwemo ODM, Wiper na Amani National Congress (ANC).

Chama cha ANC kinachoongozwa na Musalia Mudavadi kimekaribisha uamuzi huo huku kikisema kitaimarisha kampeini zake mashinani kuhakikisha kuwa muwaniaji wake Peter Nabulinda ameshinda uchaguzi huo.

Kuhusu uchaguzi wa ugavana kaunti ya Nairobi, Tuju amesema  wanasubiri uamuzi utakaotolewa na mahakama kufuatia kesi iliyowasilishwa na aliyekuwa gavana Mike Sonko.

Kiti cha useneta Machakos kilisalia wazi kufuatia kifo cha aliekuwa seneta Bonface Kabaka huku maeneo bunge ya Matungu na Kabuchai yakisalia bila wabunge kufuatia vifo vya Justus Murunga na James Lusweti mtawalio.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here