Bunge la kitaifa limetupilia mbali mswada wa marekebisho wa sheria za kudhibiti maandamano ili kuwalazimu waandalizi kuwajibikia uharibifu wowote wa mali au majeruhi.
Katika vikao ambavyo viliongozwa na naibu spika Moses Cheboi, wabunge wamezima juhudi za mwenzao wa Ruiru Simon King’ara kulazimu waandalizi kufikishwa mahakamani endapo vurugu zitatokea, watu kujeruhiwa na mali kuharibiwa.
Kiongozi wa walio wachache katika bunge hilo John Mbadi amewaongoza wabunge wenzake kupinga marekebisho hayo kwa msingi kuwa maandamano ni halali kikatiba na kuwa ni jukumu la polisi kuhakikisha kuna usalama.
Kingara na baadhi ya wabunge waliomuunga mkono wanasema marakebisho hayo yalilenga kuhakikisha kuwa hakuna uharibifu wa mali unatokea wakati wa maandamano.
Adabu inayopendekezwa kwenye mswada huo ni kifungo cha miaka sita jela au faini ya Sh100,000 kwa waandalizi wa maandamano yatakayokumbwa na ghasia.
Kimsingi, wanaoandaa maandano ni sharti wapate kibali cha Polisi ili kuhakikisha kuwa maafisa wa usalama wanakuwepo ili kutoa usalama kwa wanaoshiriki maandamano hayo.
Tukiwa bado bungeni…
Bunge la kitaifa limekashifu kubomolewa kwa makaazi ya jamii ya Wanubi eneo la Kibos kaunti ya Kisumu kwa msingi kuwa ulikiuka haki za kibinadamu.
Wakiongozwa na mbunge wa Kisumu Mashariki Shakeel Ahmed Shabbir, wabunge hao wamesema ubomozi huo ulisababisha kifo cha watoto wawili na kuwaacha maisha ya wakaazi wengi hatarini kutokana na baridi ya usiku.









