Waziri Kagwe akana kuhusika na sakata ya KEMSA

0

Kwa mara nyingine waziri wa Afya Mutahi Kagwe amejitetea kuhusiana na madai kuwa alihusika katika sakata ya kupotea kwa pesa za mlipa ushuru katika shirika la kusambaza dawa na vifaa vingine vya matibabu nchini KEMSA.

Akifika mbele ya kamati ya bunge la kitaifa kuhusu Afya, Kagwe amekiri kushauriana na afisa mkuu mtendaji aliyesimamishwa kazi wa KEMSA Dr Jonah Manjari lakini akasema hakumwagiza kwa vyovyote vile kukiuka sheria za ununuzi au kutekeleza kosa lolote.

Kagwe amesema kuwa hana uhusianao wowote na kampuni zaidi ya sitini ambazo zimekuwa zikifanya biashara na KEMSA na kusema hata haijwahi kanyaga mguu katika afisi za KEMSA.

Kagwe ameshikilia kuwa hakuna vifaa vyovyote vya msaada ambavyo vimeibwa na kuuzwa kwa taifa jirani la Tanzania na kusema bwenyenwe wa China Jack Ma aliyetoa msaada huo ameridhika na vile vilitumiwa na anapania kutuma vifaa zaidi nchini.

Kagwe anasema binafsi yake aliiendea idara ya upelelzi nchini DCI kuwataka kuchunguza iwapo kuna watu ambao walikula pesa za corona si tu katika shirika la KEMSA lakini hata katika wizara ya afya.

Kuhusiana na vifaa vya zaidi ya shilingi billion sita nukta mbili, Kagwe ameshauri vifaa hivyo kuuzwa kwa bei ya chini licha ya kununuliwa kwa bei ghali kwani bei ya vifaa hivyo katika soko la humu nchini na ulimwengu imepungua.

Wakati uo huo, maafisa wakuu katika wizara ya Uchukuzi wamefurushwa kutoka kwa kikao cha kamati ya bunge la kitaifa kuhusu Afya ambacho kinachunguza madai ya wizi wa vifaa vya msaada kupambana na janga la corona nchini.

Mwenyekiti wa kamati hiyo na mbunge wa Muranga Sabina Chege amewaagiza maafisa hao wakiongozwa na katibu mkuu Christopher Obure kurejea mbele ya kamati hiyo kesho na stakabadhi za kuonyesha jukumu lao katika usafirishaji na uhifadhi wa vifaa hivyo kutoka kwa bwenyenye Jack Ma.

Baadhi ya anachama wa kamati hiyo wamemtaka pia waziri James Macharia kufika mbele yao mwenyewe hapo kesho ili kutoa mwanga zaidi kuhusiana na sakata hiyo.

Kabla ya kufurushwa, Obure ametetea wizara ya uchukuzi kuhusiana na sakata hiyo na kusema jukumu lao lilikuwa la usafirishaji pekee.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here