Baadhi ya Wawakilishi Wadi katika Kaunti ya Kiambu wamedai kuwepo kwa njama ya kuwasilisha hoja ya kumbandua Gavana Kimani Wamatangi ofisini.
Wawakilishi wadi hao wanasema kuwa hoja hiyo inaandaliwa na watu ambao si Wawakilishi Wadi, hatua wanayodai ni kinyume na matakwa ya katiba kuhusu mchakato wa kumbandua Gavana.
Spika wa Bunge la Kaunti ya Kiambu, Charles Thiong’o, amedai kuwa ametishiwa maisha baada ya kukataa kuruhusu kuwasilishwa kwa hoja ya kumbandua Gavana Wamatangi, akisema kuwa hoja hiyo inachochewa kisiasa.
“Nina hofu na haswa kwa familia yangu kwa sababu kama mtu anataka kunidhuru anaweza kunidhuru huku nje lakini mtu anapokuja kuidhuru familia yangu nina kila sababu ya kuamini kuwa ana mipango fiche”
Haya yanajiri huku Gavana Wamatangi akikumbwa na changamoto kadhaa siku za hivi karibuni.
Miongoni mwa masaibu hayo ni kubomolewa kwa biashara zake katika uwanja wa Nyayo ili kupisha ujenzi wa kituo cha reli, Kufungwa kwa akaunti yake ya benki kwa madai ya kuhusishwa na ufisadi.
Gavana Wamatangi pia amekuwa kwenye mvutano wa kisiasa na baadhi ya wabunge kutoka Kaunti ya Kiambu wanaodaiwa kuwa wandani wa Rais William Ruto.
Miongoni mwao ni pamoja na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa, Kimani Ichung’wah, na Mbunge wa Thika mjini Alice Ng’ang’a ambaye tayari ametangaza azma ya kumbandua Gavana Wamatangi katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti.









