Shule ya Wasichana ya Njoro yafungwa kufuatia kifo cha mwanafunzi

0

Shule ya Wasichana ya Njoro katika kaunti ya Nakuru imefungwa kwa muda usiojulikana kufuatia kifo cha mwanafunzi wa kidato cha nne, Brenda Akinyi.

Familia ya marehemu Akinyi imeilaumu usimamizi wa shule hiyo kwa madai ya utepetevu, wakisema mwanafunzi huyo hakupata huduma ya haraka alipougua akiwa shuleni.

“Kufika shuleni naambiwa na marafiki zake dadako ni mgonjwa, kuuliza nani anajua mtoto ni mgonjwa, Nurse anajua eeh anajua, Matron anajua na mbona hawajapiga home simu, ati alikuwa anapewa treatment, mtoto anakuwa mgonjwa siku tatu anapewa brufein?”

Brenda alifariki dunia katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Nakuru alipokuwa akipokea matibabu.

Kwa mujibu wa familia, licha ya wazazi kuishi karibu na shule, hawakujulishwa kuwa mwanao alikuwa akiugua.

Familia inasema kuwa hatua ya kuwafahamisha ilicheleweshwa hali iliyochangia kuzorota kwa afya yake.

Shule hiyo ilifungwa leo na wanafunzi kuagizwa kurejea nyumbani, hatua iliyochukuliwa kufuatia maandamano yaliyoshuhudiwa jumatatu nje ya shule hiyo.

Wazazi na wakazi wa eneo la Njoro sasa wanadai kuwa kifo cha Brenda Akinyi si cha kwanza, wakisema kuwa takriban miaka mitatu iliyopita, mwanafunzi mwingine aliyekuwa darasa moja na marehemu pia alifariki baada ya kuugua.

Wakazi hao wanasema kuwa visa hivyo viwili vinahusishwa na utepetevu wa walimu na usimamizi wa shule, wakitaka uchunguzi wa kina ufanywe na hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here