Wanasiasa wakaidi masharti ya kuzuia msambao wa corona

0

Wanasiasa wameendelea kukaidi marufuku iliyowekwa na rais Uhuru Kenyatta kuhusu mikutano ya kisiasa katika harakati za kuzuia msambao wa virusi vya corona.

Naibu rais William Ruto, kinara wa chama cha ODM Raila Odinga pamoja na vinara wenza wa muungano wa NASA Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula wamekuwa katika mstari wa mbele kurindima ngoma la kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini pasipo kuzingatia masharti ya kuzuia corona licha ya kwamba taifa bado linaendelea kuandakisha visa vya ugonjwa huo kila siku.

Ukaidi wa masharti ya usalama kuzuia kuenea kwa virusi vya corona umeendelea kushuhudiwa huku viongozi sawa na Wakenya wakipuuza tahadhari ya watalaamu wa afya kuhusu makali ya virusi hivyo sawa na onyo lililotolewa na rais Uhuru Kenyatta mwaka jana.

Umati mkubwa wa watu ulijitokeza kumkaribisha kinara wa chama cha ODM Raila Odinga huko Githurai na Roysambu Jumatano ambapo waziri huyo mkuu alipigia debe ripoti ya BBI.

Mikutano ya Odinga ikijiri siku moja baada ya vinara wenza wa muungano wa NASA Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na Moses Wetangula kukita kambi katika kaunti ya Machakos kumpigia debe muwaniaji wa kiti cha useneta kwa tiketi ya chama cha Wiper Agnes Kavindu.

Wikendi iliyopita, naibu rais William Ruto na wendani wake walilakiwa kwa shangwe na nderemo na wananchi kule Waithaka na Kabiria eneo bunge la Dagoreti Kusini maisha yakionekana kurejelewa katika hali ya kawaida.

Na huku wanasiasa wakiwaongoza wananchi kukaidi maagizo ya kiusalama, corona ingali inasababisha maafa nchini Kenya huku visa vipya vikiendelea kuripotiwa kila kuchao.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here