Tume ya huduma za walimu nchini TSC hii leo inatazamiwa kuzindua zoezi la majaribio la kuwasajili walimu kwa mfumo wa kidijitali katika juhudi za serikali kuzima visa vya udanganyifu kwenye mitihani ya kitaifa.
Afisa mkuu mtendaji wa TSC Nancy Macharia anatazamiwa kuongoza uzinduzi huo utakaofanyika kwa vituo 143 katika kaunti 7 zilizochaguliwa.
Zoezi hilo linajumuisha kuchukua alama za vidole za walimu ambazo baadae zitawasaidia wachunguzi kunasa wanaofungua karatasi za mtihani kabla ya wakati au pia kuwapa wanafunzi simu za rununu wakati wa mitihani.
Zoezi hilo la majaribio ambalo litakamilika siku ya Ijumaa litafanyika katika kaunti za Migori, Bungoma, Uasin Gishu, Homa Bay, Kilifi, Kitui na Garissa.
Zoezi kamili lakuwasajili walimu kwa mfumo wa kidijitali litafanyika kabla ya mwishoni mwaka ujao na litaisaidia tume hiyo pia kufahamu idadi kamili ya walimu wa serikali nchini.
Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa kufikia mwaka 2019, Kenya ilikuwa na walimu 215, 363 wa shule za msingi za umma, na walimu 97,771 wa shule za upili za umma na vyuo vya mafunzo ya walimu.