Huduma za matibabu katika hospitali za umma nchini ziko hatarini kusambaratika baada ya wahudumu wa afya kushiriki mgomo kulalamikia kutolipwa mishahara yao, mikataba ya maelewano baina yao kukiukwa na pia mazingira yasiyofaa ya kazi.
KISUMU
Wahudumu wa afya isipokuwa madaktari wameanza mgomo kulalamikia kutolipwa mishahara yao.
Katibu mkuu wa muungano wa wauguzi Maurice Opetu anasema serikali ya Gavana Peter Anyang Nyongo imekataa kutii agizo la serikali kuwalipa mishahara na marupurupu yao na sasa hawana budi ila kuondoka hospitali na kupanga foleni katika afisi za serikali wakisubiri mshahara.
HOMABAY
Baadhi ya wahudumu wa afya katika kaunti ya Homabay ikiwemo madaktari na wauguzi wameapa kutorejea kazini hadi pale watakapolipwa mishahara yao.
Wahudumu hao wanasema hawajapokea mishahara yao kuanzia mwezi Aprili mwaka huu na kuongeza kuwa hawako tayari kwa mazungumzo kwani haja yao sasa ni mishahara.
Mgomo huo umedumu kwa siku kumi na tisa sasa na kusambaratisha shughuli za matibabu huku wagonjwa wakibaki bila wa kuwahudumia.
NAIROBI
Matabibu wa hospitali za umma katika kaunti ya Nairobi wametoa ilani ya kushiriki mgomo iwapo serikali haitashughulikia matakwa yao.
Mwenyekiti wa muungano wa matabibu nchini Peterson Wachira amesema wanalalamikia kucheleweshwa kwa mishahara yao na pia ukosefu wa vifaa vya kujikinga wanapohudumia wagonjwa wa virusi vya corona.
Wachira amesema kuwa wamepoteza wahudumu wa afya 16 walioambukizwa virusi vya corona.
Haya yanajiri huku madaktari katika kaunti ya Nairobi pia wakipanga kushiriki mgomo kuanzia hapo kesho kulalamikia kutolipwa mishahara yao.









