Masharti yaliyopo kuzuia msambao wa virusi vya ugonjwa wa corona yatasalia kuwepo kwa muda wa siku 60 zaidi ametangaza rais Uhuru Kenyatta.
Masharti hayo yanajumuisha kafyuu ya kutotoka nje kati ya saa nne usiku na saa kumi alfajiri na marufuku kwa mikutano ya kisiasa.
Rais Kenyatta ametangaza hili baada ya kukutana na waziri wa Afya Mutahi Kagwe na viongozi wa upinzani wakiongozwa na Raila Odinga, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula.
Rais amesema hatua hii imechochewa na kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa huo katika kaunti za Kiambu, Nyandarua, Murang’a, Makueni, Machakos, Baringo, Meru na Nyeri.
Sherehe za harusi na matanga zitahudhuriwa na watu wasiozidi 100 huku sehemu za kuabudi zikitakiwa kuzingatia masharti yaliyotolewa hapo awali na baraza linaloongozwa na askofu Anthony Muheria.
Seneta wa Baringo Gideon Moi pamoja na gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya pia walikuwepo.









