Mahakama imehairisha uamuzi kuhusu ombi maafisa wanne wa polisi wanaokabiliwa na mashtaka ya mauaji ya mtoto wa miezi sita, Samantha Pendo mwaka 2017 kuachiliwa kwa dhamana.
Uamuzi huo, uliotarajiwa kutolewa Jumatano tarehe 4 Juni 2025, sasa umetangazwa kwamba utasomwa Jumanne tarehe 10 Juni 2025, ili kutoa muda kwa pande zote husika kupokea ripoti muhimu za kabla ya dhamana na tathmini ya ulinzi kwa mashahidi.
Jaji Margaret Waringa Muigai ametoa uamuzi huo baada ya mahakama kufahamishwa kuwa ingawa ripoti hizo tayari zimewasilishwa na kutumwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) na mawakili wa maafisa hao, bado hazijafikia wadau wengine muhimu, wakiwemo wakili wa waathiriwa Willis Otieno kutoka shirika la Utu Wetu na Mamlaka ya kudhibiti utendakazi wa polisi (IPOA).
Samantha Pendo alifariki mwaka 2017 baada ya kujeruhiwa kichwani wakati wa operesheni ya polisi waliokuwa wakikabiliana na waandamanaji.









