Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetetea mchakato uliotumika kuandaa Mpango wa Uendeshaji wa Uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, ikisisitiza kuwa ulihusisha mashauriano ya kina na wadau mbalimbali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Tume na Mpango wa Uendeshaji wa Uchaguzi, Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon amesema nyaraka hizo ziliandaliwa kwa kushirikisha vyama vya kisiasa, taasisi za serikali, asasi za kiraia na wadau wengine muhimu.
“Ushirikishwaji wa umma umekuwa msingi wa maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2027.” Amesema Ethekon.
Kauli yake inajiri huku viongozi wa upinzani wakitaka kusitishwa kwa utekelezaji wa mpango huo wakidai kuwa wadau muhimu hawakushirikishwa ipasavyo katika hatua za uandaaji wake.
Wakiongozwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, viongozi hao wameibua wasiwasi kuhusu uadilifu wa sajili ya wapiga kura, matumizi ya teknolojia ya uchaguzi na mfumo wa uwasilishaji wa matokeo.
“Maandalizi ya uchaguzi yanapaswa kuwa ya wazi, jumuishi na shirikishi ili kujenga imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi.” Muturi amesisitiza.
Upinzani pia umetaka kufanyika kwa ukaguzi huru na kuimarishwa kwa mifumo ya usimamizi, huku ukiitaka IEBC kushirikisha zaidi vyama vya kisiasa, asasi za kiraia na wadau wengine kabla ya kuanza kutekeleza mpango huo.
Kwa mujibu wa viongozi hao, uaminifu wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 utategemea uwazi na uwajibikaji, wakionya kuwa kushindwa kushughulikia masuala yaliyoibuliwa kunaweza kudhoofisha imani ya wananchi katika mchakato mzima wa uchaguzi.









