Marais Watatu Afrika Mashariki Wakashifiwa Kwa Kuruhusu Ukiukaji wa Haki za Kibinadam.

0

Rais William Ruto mwenzake wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni wametuhumiwa kwa kuruhusu ukiukaji wa haki za kibinadam unaojumuisha utekaji nyara, kutoweka kwa watu kwa lazima, mateso na ukandamizaji wa sauti za upinzani katika eneo la Afrika Mashariki.

Katika taarifa yake tume ya kutetea haki za kibinadam nchini KHRC imedai kuwa viongozi hao na vyombo vya usalama katika mataifa hayo vimekuwa vikihusishwa na matukio ya kutoweka kwa wanaharakati, wanahabari na watetezi wa haki za kibinadam.

“Rais William Ruto, Rais Samia Suluhu Hassan, Rais Yoweri Museveni, Muhoozi Kainerugaba, na taasisi zote za usalama na haki za kikanda lazima wajue kwamba kutoweka kwa lazima si utawala. Utekaji nyara si utekelezaji wa sheria. Mateso si usalama wa taifa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Tume hiyo imemtaja Rais Ruto kuhusu madai ya kukamatwa kiholela na kukamatwa kwa watetezi saba wa haki za kininadam wakati wa kumbukumbu ya Juni 25.

Nchini Tanzania KHRC imemhusisha Rais Samia Suluhu Hassan na madai ya kutoweka kwa mwanaharakati David Nikindikwa huku nchini Uganda ikimtaja Rais Museveni Pamoja na mwanawe Muhoozi Kainerugaba kuhusiana na madai ya kutoweka kwa mwanaharakati Maria Matembe.

KHRC sasa imezitaka serikali za Kenya, Tanzania na Uganda kukomesha mara moja visa vya utekaji nyara na kuwafikisha mahakamani wanaozuiliwa Pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria maafisa wa polisi wanaohusishwa na vitendo hivyo.

“Viongozi wa kikanda lazima waamuru mara moja kukomesha kwa visa vya utekaji nyara na kutoweka kwa watu, vilevile kuchunguza na kuwashtaki waliohusika.”

Aidha tume hiyo imemtaka Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja, Naibu wake Eliud Lagat Pamoja na maafisa wengine wakuu wanaodaiwa kuhusika katika visa vya utekaji nyara wajiuzulu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here