Huu ndio wakati maalum, wamishenari wafuzu ‘Kairos’

0
Waratibu wa idara ya umishenari wa kanisa la AIC baada ya kufuzu (Kairos) Eldoret.

Zaidi ya wamishenari 20 kutoka kanisa la AIC Kenya wamefuzu baada ya kukamilisha mafunzo ya wiki moja kuhususiana na kazi ya umishenari kutoka kwa shirika la ‘Simply Mobilizing.’

Mafunzo hayo yalifanyika jijini Eldoret kaunti ya Uasin Gishu yakiwaleta pamoja wakilishi wa idara ya umishenari kutoka maeneo mbalimbali ya taifa yaliyojumuisha ACC za Eldoret, Bomet, Nyanza, West Pokot, Makueni na Machakos chini ya uongozi wa mkurugenzi kasisi Peter Macharia.

Akiongoza hafla ya kufuzu kwa wamishenari hao askofu wa kanisa la Africa Inland Church (AIC) Kenya Eldoret Area Church Council Dr. Luka Maiyo alisifia na kupongeza mafunzo hayo yaliyotolewa kwa madhumuni ya kuwawezesha wajumbe hao katika utendakazi.

Akiwapongeza waliofuzu, askofu Luka Maiyo alitaja mafunzo hayo kuwa hatua muhimu katika kuendeleza kazi ya umishenari akisisitiza haja ya kukumbatiwa na kuenezwa katika maeneo mengine.

‘‘Leo ni siku ya muhimu kwangu kutoa furaha ya moyo wangu kwa kupata nafasi ambayo Mungu aliandaa, huu ni mpango halisi kupitia kwa mafunzo ya ‘Kairos’ ambayo kupitia kwa mkurugenzi wetu na baraza kuu yalipangwa kuwa hapa na tuliyapokea tukijua bado kuna kazi ambayo Mungu anataka tuifanye,’’ askofu Maiyo alieleza.

‘‘Kupitia mafunzo haya tumeelewa kwamba bado kuna watu wengi na mataifa mbalimbali ambayo bado hayajamjua Yesu kama mwokozi, hivyo natoa changamoto kwa maaskofu wenzangu kwamba ni muhimu muwe na mafunzo kama haya kwenye maeneo yenu.’’ alihimiza askofu Maiyo.

Akiwa mmoja wa wakufunzi, George William Omondi ambaye ni mratibu wa kitaifa wa shirika la Simply Mobilizing Kenya linalotoa mafunzo hayo (Kairos course) ikimaanisha (wakati mwafaka) alieleza kuwa mpangilio wake ni kutoa masomo kuhusu makusudi na mpango wa Mwenyezi Mungu kutoka mwanzo hadi mwisho wa dahari na kuwawezesha wahusika kwa njia ambayo nao wataweza kuwafikia na kuwawezesha wengine.

‘‘Shirika la Simply Mobilizing ni shirika la kimataifa linaloendeshwa na maono ya kuona kuwa kila mmoja amehamasishwa kuwa katika utendakazi na Mwenyezi Mungu,” alieleza Omondi.

“Tunatumia kozi za muda mfupi kusaidia kanisa kuelewa mpango wa Mungu wa wakati maalum akisisitiza kuwa huu ndio wakati mwafaka wa kanisa kufanya kazi ya umishenari na kufikia ambao hawajafikiwa na injili.” Aliongeza.

Mafunzo haya yanayotolewa kwa zaidi ya mataifa 70 ulimwenguni yana sehemu nne kuu, biblia, historia ya umishenari, mbinu za kuwafikia wasiofikiwa, pamoja na tamaduni. Haya yote yakilenga kumchochea na kumweka muumini kuwa na mwongozo na maksudi sawa na kuelimisha kanisa kuwa na mawazo pana ya kufikia watu zaidi katika vizazi mbalimbali.

Mafunzo haya yalitolewa huku takwimu nazo zikibaini kuwa zaidi ya jamii ishirini nchini bado hazikuwa zimefikiwa na injili sawa na elfu sita duniani, ishara ya pengo kubwa la kimishenari linalohitajika kujazwa ili kuwezesha uenezaji wa injili nchini na kimataifa.

Kutokana na hili kulisisitizwa rai ya kila mmoja kujitolea kuwa mshirika katika kupiga jeki utendakazi wa umishenari kupitia michango na matoleo mbalimbali.

Mwenyekiti wa AIC MD eneo la Eldoret West kasisi William Soimo ailipongeza mafunzo hayo na kuyataja kama yaliyokuja kwa wakati na kubadilisha mtazamo kuhusu kazi ya umishenari kwa kujua kwamba walengwa ni wale ambao hawajafikiwa “the unreached” kinyume na hali ambapo wengi hujipata wamelenga maeneo ambayo tayari yamefikiwa na injili “the reached.”

‘‘Ukiangalia katika makanisa mengi utapata kwamba wamishenari wao wako katika maeneo ambayo tayari yamefikiwa na tumepata changamoto kujua kwamba tunafaa kwenda mahali ambapo watu hawajapata neno la Mungu au hata dini yenye mafunzo ya kweli.’’

Akitolea mfano kanisa la AIC K kama lililojengwa kwa misingi ya umishenari, kasisi Soimo aliwarai wakristo kwa jumla kuwa wa baraka kwa wasiofikiwa na injili huku akimshukuru Mungu kwa kila ambaye amekuwa akitoa mchango wa aina mbalimbali kuhakikisha kuwa wamishenari wanaendeleza utume mkuu kama ilivyoamriwa katika Biblia (Marko 16:15)

Kasisi Stephen Munguti aliyewakilisha eneo la Machakos kwa upande mwingine alieleza msukumo alioupata wa kuchochea mafunzo hayo katika maeneo ya huduma ili kuafikia uenezaji wa injili ya Kristo kwa jamii ambazo zingali kufikiwa, kauli iliyosisitizwa na Daniel Muthana wa eneo la Makueni Central.

‘‘Mafunzo haya yamenisaidia sana kwa upande wa umishenari ambapo awali kuna mengi ambayo sikuwa nikiyafahamu ila sasa kuna mengi nimeyafahamu ambayo tunafaa kuyatekeleza kama kanisa ikiwamo kuombea wamishenari, na hata kuwawezesha kwa njia mbalimbali. Ninapotoka hapa haya mafundisho nitayafundisha kanisani na pia nitahamasisha eneo pana ninalohudumu kwa ujumla.” Alisisitiza Munguti.

Wakiwa wamewezeshwa, wajumbe waliofuzu walitaja mafunzo hayo kuwa mwamko mpya na changamoto kwao, kusudi likiwa kuwezesha na kumruhusu aliyewezeshwa kumfikia mwingine ili kufikia hitaji lililopo la kuhubiria mataifa ambayo bado hayajapata fursa ya kuhubiriwa.

 

 

 

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here