IEBC Yatoa Ratiba ya Uchaguzi wa 2027, Maafisa wa Umma Kujiuzulu Kufikia Februari 9.

0

Uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027 utafanyika mnamo siku ya Jumanne, Agosti 10, 2027.

Haya ni kwa mujibu wa Kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini IEBC na Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa Uchaguzi, Ann Nderitu.

Nderitu amesisitiza kwamba tarehe hiyo imedhibitishwa hivyo haiwezi kubadilika kivyovyote vile.

Aidha amesema kuwa Maafisa wa umma wanaonuia kuwania nyadhifa mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 watalazimika kujiuzulu ifikapo Februari 9, 2027, miezi sita kabla ya uchaguzi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa IEBC na Mpango wa Uendeshaji wa Uchaguzi, Nderitu amesema vyama vya kisiasa vinavyonuia kuwasimamisha wagombea vitatakiwa kuwasilisha orodha ya wanachama wao, majina ya wanaotarajia kushiriki kura za mchujo pamoja na tarehe na maeneo ya kura hizo ifikapo Machi 16, 2027.

Aidha, vyama hivyo vitapaswa kukamilisha kura za mchujo na kutatua mizozo ya ndani kufikia Mei 9, 2027.

Kwa upande wa wagombea huru, Nderitu amesema hawapaswi kuwa wanachama wa chama chochote cha kisiasa kufikia Mei 9, 2027, na wanatakiwa kuwasilisha majina na alama watakazotumia kwenye uchaguzi ifikapo tarehe hiyo.

Uteuzi wa wagombea wa vyama vya kisiasa na huru utafanyika kati ya Mei 29 na Juni 11, 2027, huku mizozo yote ya uteuzi ikitakiwa kuwasilishwa kabla ya Juni 12 na kutatuliwa ndani ya siku kumi.

Aidha amesema kipindi rasmi cha kampeni kitaanza Mei 29, 2027 na kuhitimishwa Agosti 7, siku mbili kabla ya uchaguzi. Kampeni hizo zikiruhusiwa kuanzia saa moja asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni.

Aidha ameeleza kuwa Tume hiyo inakusudia kufanya zoezi jingine la Usajili wa wapiga kura wapya kabla ya mwisho wa mwaka huu na mwanzoni mwa mwaka ujao.

“Tunapanga kufanya zoezi jingine la uandikishaji wa wapiga kura kabla ya mwisho wa mwaka huu na mwanzoni mwa mwaka ujao,” amesema Nderitu.

Wakati uo huo amefichua kuwa IEBC ilisajili wapiga kura milioni 2.6 kupitia zoezi la usajili endelevu na kampeni maalum za usajili.

Kadhalika amedhibitisha kuwa lengo la tume hiyo ni kufikisha idadi ya wapiga kura wapya milioni 6.3 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

“Tumedhamiria kuhakikisha kila Mkenya anapata fursa ya kujiandikisha na kushiriki katika mchakato wa kidemokrasia,” ameongeza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here