Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko atalala kwenye seli za Polisi kwa siku mbili zaidi baada ya mahakama ya Kiambu kukataa kumuachiliwa kwa dhamana.
Hakimu wa mahakama hiyo Stellah Atambo ametoa agizo hilo ili kufanikisha kukamilika kwa uchunguzi dhidi yake baada ya kukanusha mashtaka kumi na mawili.
Mashtaka hayo ni pamoja na kumsababishia mtu majereha, kupanga vurugu, wizi wa kimabavu pamoja na uharibifu wa mali unaohusishwa na kuingia kwa nguvu kwa mali ya kibinafsi katika mtaa wa Buruburu.
Upande wa mashtaka unataka gavana huyo kupelekwa katika mahakama Mombasa ambako waranti ya kukamatwa ilitolewa dhidi yake.
Sonko anatuhumiwa kumjeruhi Alex Kioko na kumsababishia majeraha ya mwili na pia yeye pamoja na wengine ambao hawakuwa mahakamani walimuumiza Musyoki Kavunda na John Mungai katika mtaa huo.
Sonko alikesha katika kituo cha polisi cha Muthaiga baada ya kuhojiwa Jumatatu.
Katibu katika wizara ya usalama wa ndani Karanja KIbicho alimshtaki Sonko kwa DCI pia kwa madai ya kumchafulia jina alipomhusisha na ghasia hizo









