Seneta Yusuf Hajji azikwa Lang’ata

0

Aliyekuwa Seneta wa Garissa Yusuf Hajji amezikwa Jumatatu jioni katika makaburi ya Waislamu ya Lang’ata baada ya kifo chake kutangazwa asubuhi akiwa na umri wa miaka 80.

Hafla hiyo ya mazishi imehudhuriwa na rais Uhuru Kenyatta, naibu wake William Ruto, kinara wa chama cha ODM Raila Odinga pamoja na viongozi wengine.

Yusuf Hajji anapumzishwa saa chache baada ya kufariki dunia kutokana na kuugua kwa muda mrefu.

Katika rambirambi zake, Rais Uhuru Kenyatta amemtaja Haji kama kiongozi wa kutegemewa na mzalendo huku akitaja kifo chake kama pigo kwa taifa.

Kenyatta amesema Kenya itakosa uongozi wa Haji haswa katika mchakato wa BBI na kuiombea familia yake faraja.

Mawaziri Najib Balala (Utalii), Monica Juma (Ulinzi) na Ukur Yattani (Fedha) wamemtaja taifa hili limempoteza kiongozi aliyechapa kazi kwa kujitolea.

Viongozi wengine akiwemo seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Jr wametaja mchakato wa kurekebisha katiba kupitia BBI kama mchango wake wa hivi punde katika taifa hili ikizingatiwa kwamba aliongoza jopokazi lililobuni ripoti ya BBI.

Haji alikuwa waziri wa usalama wa ndani kutoka mwaka wa 2008-2013 wakati wa serikali ya mseto.

Alichaguliwa mwaka 2013 kuwa seneta wa Garissa na kuingia bungeni ambapo amehudumu katika kamati mbalimbali ikiwemo ile ya usalama.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here