Madiwani wa chama cha KANU katika kaunti ya Baringo wamewasilisha kesi mahakamani kupinga namna mchakato wa kukataliwa kwa mswada wa BBI ulivyoendeshwa.
Wakizungumza baada ya kuwasilisha kesi katika mahakama kuu ya Kabarnet, madiwani hao wakiongozwa na wakili wao Gordon Ogola wamesema bunge hilo lilikosa kufuata sheria wakati wa mjadala huo ulioishia kukatalia mbali mswada huo.
Diwani mteule Betty Birchogo anadai kuwa maoni ya wenyeji hayakujumuishwa kwenye mswada huo akilaumu kamati ya bunge hilo kuhusu haki na maswala ya kisheria kwa kuharakisha mjadala huo pasipo maoni hayo.
Kwenye vikao vilivyokumbwa na vurugu, mswada huo ulipingwa na madiwani 30 na kuungwa mkono na madiwani 11 na kufanya bunge la kaunti ya Baringo kuwa la kwanza kukataa kupitisha mswada huo.