Wanariadha wa masafa marefu wa Kenya, Sabastian Sawe na Agnes Ngetich, wameorodheshwa kuwania tuzo za mwanariadha bora wa dunia mwaka 2026 kwa upande wa wanaume na wanawake, mtawalia.
Shirikisho la Riadha Duniani, Jumanne tarehe 6 Oktoba, lilitangaza orodha ya wanariadha 20 wawaniaji wa tuzo hizo, kabla ya hafla ya ‘World Athletics Awards’ itakayofanyika jijini Monaco, Ufaranza tarehe 27 Novemba.
Sawe, ambaye aliweka historia kwa kuwa mwanaume wa kwanza kukimbia marathoni kwa muda wa chini ya saa mbili katika mashindano rasmi, aliweka rekodi mpya ya dunia ya saa 1:59:30 katika mbio za London.
Sawe anatarajiwa kukabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wanariadha wengine, akiwemo nyota wa Sweden, Mondo Duplantis, ambaye aliiboresha rekodi yake ya dunia ya kuruka kwa kutumia mti hadi mita 6.31 na kushinda mataji ya ‘Ultimate, World indoor na European’.
Kwa upande wa tuzo za wanawake, Ngetich alishinda taji la dunia la mbio za nusu marathoni kwa tofauti ya sekunde 50, akiweka rekodi ya dunia ya wanawake pekee ya saa 1:05:15, pia alishinda taji la dunia la mbio za nyika kwa tofauti ya sekunde 42, aliweka muda bora zaidi duniani wa dakika 8:08.95 katika mbio za mita 3,000 na dakika 28:58 katika mbio za kilomita 10.
Ngetich anaungana katika orodha hiyo na wanariadha wengine, akiwemo raia wa Ethiopia Tigst Assefa, aliyeshinda ‘Berlin Marathon’ kwa muda wa saa 2:11:04, ambao ni muda wa tatu kwa kasi zaidi katika historia, pamoja na ‘London Marathon’ kwa rekodi ya dunia ya wanawake pekee ya saa 2:15:41.
Washindi sita wa mwisho, watatu katika tuzo ya mwanariadha bora wa dunia kwa wanawake na watatu kwa wanaume watatangazwa tarehe 10 na 11 Novemba na wataalikwa Monaco kwa hafla ya ‘World Athletics Awards’ tarehe 29 Novemba, ambapo kila mshindi atatangazwa moja kwa moja jukwaani.
Jopo la wataalamu wanane wa takwimu, wawili kutoka shirikisho la riadha duniani na mmoja kutoka kila moja ya vyama sita vya kikanda lilichagua wanaowania tuzo hizo.
Kura itakayoamua mshindi itapigwa na mashabiki, wanariadha, wanahabari, na shirikisho ambayo itafungwa Jumamosi, Oktoba 17 saa sita usiku.
Tuzo nyingine zitakazotolewa jukwaani ni pamoja na tuzo za mwanariadha chipukizi bora kwa wanaume na wanawake, kocha bora wa mwaka, tuzo ya rais, pamoja na tuzo mpya ya tukio bora la mwaka, ambayo itatolewa kwa mara ya kwanza.









