Kenya Haina Mlipuko wa Ebola Waziri Duale Ahakikisha.

0

Kenya haina mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Ebola, ni hakikisho lililotolewa na Waziri wa Afya Aden Duale

Duale amefafanua kuwa kisa kilichoripotiwa ni tukio linalomhusisha mtu aliyeingia nchini akiwa tayari ameambukizwa ugonjwa huo baada ya kusafiri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

“Kenya haina mlipuko wa Ebola. Kilichotokea ni kisa cha Ebola kilichoingizwa nchini, sawa na visa vilivyoripotiwa nchini Ujerumani na Ufaransa,” amefafanuaDuale.

Amesema Serikali imechukua hatua zinazohitajika kukabiliana na hali hiyo, akisisitiza kuwa Kenya iko tayari, tofauti na hali iliyoshuhudiwa mwanzoni mwa janga la Corona.

Kwa mujibu wa Waziri wa Afya Aden Duale, takriban abiria 650,000 wamefanyiwa uchunguzi katika vituo 15 vya kuingia nchini kama sehemu ya hatua za kuzuia kuenea kwa Ebola.

Duale amesema wahudumu wa afya 4,900 wamepewa mafunzo ya kushughulikia visa vya Ebola, huku visa 276 vilivyoshukiwa kuwa vya Ebola vikifanyiwa uchunguzi na kunainika kuwa havikuwa na virusi hivyo.

Duale amesema mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na Ebola nchini alifuatiliwa kutoka safari yake katika Eneo la kaskazini-magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kupitia miji kadhaa hadi kuingia Kenya.

“Mgonjwa huyu aliingizwa nchini kwa sababu tunaweza kufuatilia safari yake, jinsi alivyotoka kaskazini-magharibi mwa Congo, DRC, hadi Kisangani, Beni, Kinshasa, Kampala na hatimaye Kenya,” ameeleza.

Duale pia amedokeza kuwa dawa ambazo mgonjwa huyo alikuwa akitumia akiwa safarini huenda ziliathiri uwezo wa mashine za kupima joto katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kumtambua.

“Alipoingia Kenya alikuwa akitumia dawa na huenda alitumia dawa nzito zilizomsaidia kutogunduliwa na mashine zetu za kupima joto katika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA,” amesema.

Wizara ya Afya imesema kisa hicho kinashughulikiwa kupitia mifumo iliyopo ya ufuatiliaji na kukabiliana na magonjwa, huku mamlaka za afya zikiendelea kuwafuatilia watu waliokutana na mgonjwa huyo na kuimarisha ukaguzi katika vituo vya kuingilia nchini.

Wakati uo huo Waziri Duale amesema kituo cha karantini cha Laikipia kinaweza kubadilishwa kuwa hospitali kubwa ya magonjwa ya kuambukiza iwapo serikali itapata idhini ya mahakama.

Duale amesema kituo hicho, ambacho awali kilipangwa kuwa na vitanda 50 na hadhi ya Level Six, kinaweza kupanuliwa hadi vitanda 200 au 300.

Amesema serikali pia inapanga kushirikiana na Marekani kukiendeleza kituo hicho kuwa hospitali ya kikanda ya magonjwa ya kuambukiza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here