Wanasiasa Waonywa Dhidi ya Kutumia Wahuni Kuvuruga Amani.

0

 

Waziri mwenye mamlaka Makuu Musalia Mudavadi amewaonya wanasiasa dhidi ya kutumia makundi ya wahuni kuvuruga amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027

Akizungumza wakati wa mkutano wa pili wa Kamati ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Maendeleo wa mwaka 2026 tarehe 12 Oktoba, Mudavadi amesisitiza kuwa wote watakaohusika katika vitendo vinavyotishia usalama watawajibishwa kwa mujibu wa sheria bila kujali misimamo yao ya kisiasa.

Mudavadi amesema serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Asasi za usalama ili kuhakikisha vitisho vinavyoweza kuvuruga amani vinatambuliwa na kushughulikiwa mapema kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

“Tunaimarisha ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali ili kuhakikisha vitisho vinavyojitokeza dhidi ya amani vinatambuliwa na kushughulikiwa mapema, kabla ya siku ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi,” amesema Mudavadi.

Ameongeza kuwa yeyote anayetishia amani na usalama atawajibishwa bila kujali uhusiano wake wa kisiasa au hadhi yake katika jamii, akisisitiza kuwa serikali lazima ilinde wananchi, taasisi na miundombinu muhimu kwa uchaguzi wa kuaminika.

“Lazima tuchukue hatua dhidi ya wote wanaotishia amani na usalama, wawe marafiki, majirani au jamaa zetu. Waonywe wazi kuwa watawajibishwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria, bila kujali hadhi yao katika jamii au misimamo yao ya kisiasa.” Ameeleza.

Mudavadi pia amewakosoa wanasiasa wanaodokeza kuwa uchaguzi wa mwaka 2027 unaweza kuibwa au matokeo kuhitilafiwa akionya kuwa kauli hizo zinaweza kuzua mashaka miongoni mwa wananchi kuhusu uadilifu wa mchakato wa uchaguzi.

“Mtu anaposema ‘tutaiba, tutajaza’, inaweza kuonekana kama kauli ndogo tu, lakini anayetoa kauli hiyo ni mtu mwenye ushawishi mkubwa katika jamii.” Ameongeza.

“Rais ana kila nia ya kushinda kupitia mchakato huru na wa haki, na hataki kujihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu,” ameelezea Mudavadi.

Aidha, Mudavadi amesisitiza kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) lazima iruhusiwe kutekeleza majukumu yake ya kikatiba kwa uhuru, akionya dhidi ya juhudi za kuidharau au kudhoofisha imani ya umma katika tume hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here