Safari ya Marekani iligharimu shilingi milioni kumi pekee rais Ruto asema

0
RAIS WILLIAM RUTO AKISAFIRI MAREKANI

Kwa mara nyingine rais William Ruto ametetea gharama ya safari yake nchini Marekani juma lililopita baada ya kudaiwa kuwa ya juu zaidi.

Katika hotuba yake alipoongoza hafla ya maombi ya kitaifa siku ya Alhamisi, rais Ruto ameeleza kwamba alikodi ndege aliyoitumia kwa safari hiyo kutoka kwa marafiki zake kwa gharama ya shilingi milioni kumi pekee.

 ‘‘Acha niweke wazi hapa kwamba iligharimu serikali ya Kenya chini ya shilingi milioni kumi, nilipoambiwa ndege ya gharama ya chini ni shilingi milioni sabini niliambia ofisi yangu iagize ndege ya shirika la Kenya airways, baadhi ya marafiki zangu walipopata habari kwamba ningetumia ndege ya Kenya airways wakaniuliza kiwango cha fedha nilichokusudia kulipa nikawaambia sikuwa tayari kulipa zaidi ya milioni ishirini, hapo ndipo wakaniambia leta shilingi milioni kumi tutakupa ndege.’’ Amefafanua rais Ruto.

 Kiongozi wa taifa pia amesisitiza kwamba ataendelea kuongoza akiwa kwenye mstari wa mbele katika matumizi yanayofaa ya fedha za umma akiwataka wanaoendeleza mazugumzo hayo kukoma.

Kadhalika amri jeshi mkuu amesema kwamba serikali yake itahakikisha kwamba katika kipindi cha miaka mitatu ijayo hakutakuwapo na upungufu katika bajeti.

Kauli ya rais inajiri kufuatia mjadala ulioibuka nchini kuhusu kiwango cha fedha alichokitumia kwenye safari hiyo ikidaiwa kwamba iligharimu shilingi milioni mia mbili madai ambayo ameyapuuza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here