Rais William Ruto amesema serikali haitaruhusu tena wanasiasa kuingilia au kuvuruga uongozi wa bodi za mashirika ya umma yaliyoorodheshwa katika soko la hisa.
Akizungumza wakati wa kuorodheshwa rasmi kwa kampuni ya Kenya Pipeline (KPC) katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE), Rais amesema ni muhimu kulinda mashirika hayo dhidi ya ushawishi wa kisiasa ili yaweze kufanya kazi kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji.
Rais aidha amekosoa utaratibu wa zamani ambapo wanasiasa waliopoteza uchaguzi waliteuliwa kujiunga na bodi za mashirika ya umma, akisema hali hiyo imekuwa ikiathiri utendaji wa taasisi hizo.
“Iwapo mtu atashindwa katika uchaguzi, siku inayofuata tunamteua kuwa mjumbe wa bodi ya Kenya Pipeline. Anapofika huko, jambo la kwanza analotafuta ni pesa, na tunaharibu kabisa mfumo mzima. Hilo litakuwa jambo la zamani,” alisema Rais Ruto.
Aidha, Rais amesema kuwa mapato ya awali ya takriban shilingi bilioni 106 yaliyopatikana kupitia utoaji wa hisa wa kampuni ya Kenya Pipeline yatafungua njia ya kupata takriban shilingi trilioni 1.2 zitakazosaidia kufadhili miradi mbalimbali ya miundombinu nchini kupitia hazina ya kitaifa ya miundombinu.
“Shilingi bilioni 106 tulizokusanya kupitia IPO hii zinatupa fursa ya kupata takriban shilingi trilioni 1.2 ambazo zitatusaidia kubadilisha na kuimarisha miradi mingi ya miundombinu nchini,” aliongeza Rais.
Wakati huo huo, Waziri wa Fedha John Mbadi amepuuzilia mbali madai ya baadhi ya wakosoaji waliokuwa wakitilia shaka mafanikio ya utoaji wa hisa wa kampuni ya Kenya Pipeline.
Mbadi amesema kuwa hatua hiyo imefanikiwa licha ya kukashifiwa kwa mpango huo na wale waliodai kuwa haungefaulu.
“Licha ya kuwepo kwa wale waliokuwa wakitabiri kushindwa kwa mpango huu, utoaji wa hisa wa Kenya Pipeline umefanikiwa na umeonyesha imani ya wawekezaji katika soko letu la hisa,” alisema Mbadi.









