Mahakama Kuu ya Kibera Yamruhusu Samson Talaam Kupata Matibabu KNH

0

Mahakama Kuu ya Kibera imemruhusu aliyekuwa mkuu wa kituo cha polisi cha Central, Samson Talaam, kutafuta huduma za matibabu katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta.

Talaam amekuwa akizuiliwa tangu kushtakiwa kwake mnamo mwezi wa Juni 13, 2025 kufuatia kifo cha mwanablogu na mwalimu Albert Ojwang’, aliyefariki akiwa mikononi mwa polisi katika kituo cha Central.

Kifo hicho kilizua maandamano makubwa jijini Nairobi, huku waandamanaji wakishinikiza haki ipatikane.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Diana Kavedza aliwaagiza maafisa wa gereza kuhakikisha Talaam anapelekwa hospitalini ili kupata huduma zinazohitajika.

Katika kikao cha mahakama mnamo mwezi Machi 11, 2026, wakili wa Talaam, Stanley Kangai, alieleza kuwa mteja wake anakabiliwa na matatizo ya figo na anahitaji matibabu ya haraka.

Mahakama iliagiza kuwa Talaam apelekwe hospitalini kwa uchunguzi na matibabu, na kutaka ripoti ya matibabu iwasilishwe mahakamani baada ya tathmini hiyo.

“Maafisa wa gereza wanapaswa kuhakikisha mshtakiwa amepelekwa Hospitalini kwa uchunguzi na matibabu, kisha ripoti ya matibabu iwasilishwe mahakamani baada ya uchunguzi huo,” Jaji Kavedza aliamuru.

Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 17 Machi 2026 kwa maelekezo zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here