Ubalozi wa Urusi nchini Kenya umethibitisha kuwa raia sita waliuawa na wengine 37 kujeruhiwa baada ya shambulio la kombora kugonga mji wa Bryansk, Urusi katika mashambulizi ya hivi karibuni katika mzozo wa Urusi na Ukraine.
Katika taarifa iliyotolewa mnamo Machi tarehe 11, 2026 ubalozi umesema kwamba shambulio la kombora lilifanywa na Ukraine na kudai kuwa liliwalenga raia kimakusudi huko Bryansk, mji ulioko magharibi mwa Urusi karibu na mpaka na Ukraine.
“Raia 6 wameuawa na 37 kujeruhiwa katika shambulio la kombora la Ukraine katika mji wa Bryansk nchini Urusi. Utawala wa Kiev uliwalenga raia kimakusudi,” umesema Ubalozi wa Urusi.
Licha ya kuthibitisha majeruhi, ujumbe wa kidiplomasia wa Urusi jijini Nairobi haukuweza kubaini mara moja kama kuna raia yeyote wa Kenya waliokuwa miongoni mwa waathiriwa waliouawa wakati wa shambulio hilo lililosababisha majeraha.
Tukio hili linajiri wakati ambapo wasiwasi unaongezeka miongoni mwa familia za Wakenya ambao jamaa zao walisafiri hadi Urusi baada ya kuajiriwa kupigana katika vita vinavyoendelea vya Urusi na Ukraine.
Ripoti za kijasusi zilizowasilishwa bungeni mnamo Februari 18, 2026 na Kiongozi wa wengi kwenye bunge la Kitaifa Kimani Ichungwa kufuatia taarifa kutoka kwa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) zilionyesha kuwa zaidi ya Wakenya 1,000 waliajiriwa kinyume cha sheria katika jeshi la Urusi baada ya kuahidiwa mishahara minene.
Ripoti hiyo ilionyesha kuwa waajiriwa walivutiwa na mapato ya kila mwezi ya hadi Ksh350,000 na bonasi za ziada zinazozidi Ksh1.2 milioni.
Taarifa zaidi zilizowasilishwa kwa idara ya Upelelezi wa makosa ya Jinai (DCI) mnamo Februari 8, 2026 zilionyesha kuwa angalau Wakenya 200 walikuwa tayari wametumwa katika mapigano hayo ya Urusi dhidi ya Ukraine.
Wakati uo huo, Katibu Mkuu wa Masuala ya Kigeni wa Kenya Korir Singoei amefanya mikutano na wanadiplomasia wa Urusi na Ukraine jijini Nairobi ili kuangazia njia zinazowezekana za kuwafuatilia na kuwarudisha nyumbani raia wa Kenya walioathiriwa na mzozo huo.









