Mahakama Kuu imetoa agizo la muda la kuizuia Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) kutekeleza mfumo wa utozaji wa faini za papo hapo kwa madereva wanaokiuka sheria za trafiki.
Katika uamuzi wake, Jaji Bahati Mwamuye ametoa amri ya kusitisha utekelezaji wa mfumo huo mpya hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani isikilizwe na kuamuliwa kikamilifu. Kesi hiyo iliwasilishwa na wakili Shadrack Wambui, ambaye anapinga uhalali wa hatua hiyo ya NTSA.
“Mahakama hii inatoa amri ya muda ya kuzuia utekelezaji wa mfumo wa utoaji wa faini za papo hapo au mfumo mwingine wowote wa kufanya maamuzi ya mara moja katika usimamizi wa makosa ya trafiki hadi pale ombi lililowasilishwa litakaposikilizwa na kuamuliwa,” Jaji Mwamuye ameamuru.
Uamuzi huo unamaanisha kuwa NTSA pamoja na taasisi nyingine zinazohusika hazitaruhusiwa kwa sasa kutoa au kutekeleza adhabu za trafiki kupitia mfumo huo.
Wakati uo huo, mahakama pia imeangazia wasiwasi uliotolewa kuhusu uteuzi wa benki moja kupokea malipo ya faini hizo. Kwa mujibu wa uamuzi huo, benki iliyotajwa sasa itajumuishwa rasmi kama mhusika katika kesi hiyo ili kutoa ufafanuzi kuhusu jukumu lake.
“Kwa kuzingatia masuala yaliyoibuliwa kuhusu usimamizi na ukusanyaji wa faini hizo, mahakama inaagiza taasisi ya kifedha iliyotajwa ijumuishwe mara moja kama mhusika katika shauri hili ili iweze kutoa maelezo yanayohitajika,” imesema sehemu ya uamuzi wa mahakama.
Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena tarehe 9 Aprili 2026, ambapo itathibitisha iwapo pande zote zimezingatia maagizo yaliyotolewa na kutoa mwelekeo kuhusu hatua inayofuata katika usikilizaji wa ombi hilo.
Mfumo huo mpya uliokuwa umeanzishwa chini ya Sheria za Trafiki na Makosa Madogo za mwaka 2016 ulikusudia kuwaruhusu madereva waliobainika kufanya makosa madogo ya barabarani kulipa faini mara moja badala ya kupitia mchakato mrefu wa mahakama.
Kwa mujibu wa NTSA, hatua hiyo ilikuwa sehemu ya mikakati ya kuboresha utekelezaji wa sheria za trafiki, kupunguza msongamano wa kesi mahakamani na kuimarisha uwajibikaji wa watumiaji wa barabara kote nchini.









