Rais Uhuru Kenyatta ameongoza taifa kumwomboleza aliyekuwa mbunge wa Juja Francis Munyua Waititu aliyefariki baada ya kuugua saratani ya ubongo.
Katika rambirambi zake, Rais Kenyatta amesema taifa limepoteza kiongozi jasiri na aliyejitolea kuleta maendeleo haswa katika eneobunge lake.
Rais Kenyatta amesema Wakapee, alivyofahamika na wafuasi wake, atakumbukwa kutokana na juhudi zake za kupigana na saratani nchini kwa kushinikiza kupunguzwa kwa gharama ya matibabu.
Spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi amewaongoza wabunge kumwomboleza Wakapee na kusema atakumbukwa kutokana na juhudi zake kuboresha sekta ya Kilimo na pia kuwawezesha wakenya kufanya biashara kwenye mazingira bora.
Wakapee alifariki akipokea matibabu katika hospitali ya MP Shah, jijini Nairobi.
Wakapee aligonga vichwa vya habari mwaka 2018 wakati alidokeza kuwa zaidi ya wabunge 60 walikuwa wanaugua saratani.