Rais Uhuru Kenyatta amekutana na maafisa wa ngazi za juu serikalini kujadili kulikofikia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Mkutano huo uliwaleta pamoja mawaziri, makatibu wakuu pamoja na makatibu wasaidizi kutathmini mipangilio ya serikali katika kuafikia Ajenda Nne kuu za serikali.
Msemaji wa Ikulu Kanze Dena katika taarifa ameelezea kuwa rais Kenyatta alitumia fursa hiyo kuweka wazi maono yake mwaka huu kuu ikiwa ni kukamilishwa kwa miradi mbalimbali inayoendelea katika sehemu zote nchini.
Rais Kenyatta vile vile amewaagiza maafisa hao kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali za umma akisema Wakenya wanahitaji kupata matokeo mema wakati pesa zao zinatumika.
Amewasihi kukumbatia ushirikiano na umoja ili kuafikia malengo ya kuwahudumia Wakenya na ahadi ambazo serikali ilitoa kwa wananchi.
Mkutano huu ambao haukuhudhuriwa na naibu rais William Ruto unajiri wakati ambapo mawaziri wakiongozwa na Fred Matiang’i wa usalama wa ndani wamekuwa wakizuru maeneo mbalimbali nchini kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo barabara.