Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ametangaza kujiondoa katika chama tawala cha UDA na kujiunga na upinzani, kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027.
Nyoro alitoa tangazo hilo usiku wa Jumatatu Agosti 17 wakati wa kikao na wanahabari jijini Nairobi.
Nyoro amesema ameunda chama chake cha People’s Party of Kenya baada ya kufanya mashauriano na viongozi mbalimbali kuhusu mwelekeo wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Kulingana na Nyoro, amekuwa akifanya mashauriano na viongozi kadhaa wa upinzani, akiwemo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kiongozi wa chama cha Peoples Liberation Party PLP Martha Karua, aliyekuwa Waziri Peter Munya, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Gavana wa Siaya James Orengo na aliyekuwa Waziri Justin Muturi.
“Nimechukua muda kushauriana na karibu viongozi wote wa upinzani.” amesema Nyoro.
Nyoro amesema uzoefu wake serikalini ulimpa fursa ya kutathmini hali ya nchi katika sekta mbalimbali na kubaini maeneo yanayohitaji mabadiliko.
Amesema pia ataanza ziara za kisiasa katika kaunti mbalimbali nchini, akitaja Uasin Gishu, Nandi, Bomet, Elgeyo Marakwet na Kericho miongoni mwa maeneo atakayoyazuru.
Amesema ziara hizo zitampa fursa ya kuzungumza na Wakenya kuhusu utendakazi wa serikali waliyoichagua mwaka 2022.
“Mnajua kazi niliyofanya tulipokuwa tukimsaidia hata Rais anayekalia kiti kwa sasa,” amesema Nyoro.”
“Nitakuja kuwaeleza kwa nini, baada ya kufanya kazi yote hiyo, tumefikia hatua hii. Kwa nini sasa tunahama kuelekea Upinzani”
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, Nyoro alichaguliwa kuwa Mbunge wa Kiharu kupitia tiketi ya chama cha UDA na alikuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa katika serikali ya Kenya Kwanza.









