Gachagua Ahamia Mahakama ya Rufaa Kupinga Kuondolewa Madarakani.

0

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amewasilisha rufaa katika Mahakama ya Rufaa akitaka kubatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu uliothibitisha kuondolewa kwake madarakani.

Gachagua amepinga uamuzi wa jopo la majaji watatu, Eric Ogola, Antony Mrima na Fredah Mugambi, ambao walishikilia kuwa uamuzi wa Seneti wa kumuondoa madarakani ulikuwa wa mwisho.

Anasema Mahakama Kuu ilikiri kuwa baadhi ya hatua za mchakato huo zilikiuka haki yake ya kusikilizwa, akisisitiza kuwa haki za kikatiba haziwezi kupuuzwa kwa sababu ya muda uliowekwa wa kufuata taratibu au masuala ya kisiasa.

“Haki za kikatiba haziwezi kupuuzwa kwa sababu ya muda uliowekwa wa kufuata taratibu au masuala ya kisiasa.” Gachagua amesema katika nyaraka alizowasilisha mahakamani.

Katika rufaa hiyo, Gachagua pia anapinga tafsiri ya Kifungu cha 145 cha Katiba, kinachoeleza utaratibu wa kumuondoa Naibu Rais madarakani.

Aidha, anadai kuwa Bunge la Kitaifa na Seneti hazikutoa fursa ya kutosha kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kumuondoa madarakani huku akipinga uamuzi kuhusu kuidhinishwa kwa Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais, akisema ushiriki wa umma ulipaswa kuzingatiwa katika mchakato huo.

Gachagua pia amedai kuna tofauti kati ya uamuzi uliosomwa hadharani na nakala ya maandishi iliyotolewa baadaye.

Kwa mujibu wake, majaji walisoma aya nne za ziada wakati wa kutangaza uamuzi huo, lakini hazikuonekana katika nakala ya mwisho.

Wakati huo amepinga fidia ya shilingi milioni 50 aliyopewa kwa kukiukwa kwa haki zake za kikatiba, akisema kiasi hicho hakikutosha kwa kuwa Mahakama Kuu haikutangaza mchakato wa kumuondoa madarakani kuwa kinyume cha Katiba.

Sasa anaitaka Mahakama ya Rufaa itangaze uamuzi wa Seneti wa Oktoba 17, 2024, wa kumuondoa madarakani kuwa kinyume cha Katiba na batili.

Pia anataka Msajili wa Mahakama Kuu aelekezwe kurekebisha rekodi ya uamuzi huo kwa kuingiza aya anazodai ziliachwa katika nakala ya mwisho, pamoja na kulipwa gharama za rufaa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here