Naibu Kiongozi wa Chama cha Jubilee Fred Matiang’i, ameikashifu serikali kwa madai ya kutumia vurugu kuwa silaha ya kisiasa na kujilinda madarakani.
Akizungumza katika makao makuu ya Jubilee jijini Nairobi Jumatatu Agosti 17, 2026 kuhusiana na ghasia zilizoshuhudiwa kwenye Mkutano wa Vuguvugu la Linda Mwananchi katika kaunti ya Homabay, Matiang’i amesema hakuna namna vurugu hizo zingetokea bila serikali kuwa na taarifa za awali
Kulingana na Matiang’i, mashambulizi dhidi ya wafuasi wa Linda Mwananchi yalipangwa mapema akisema mienendo ya baadhi ya maafisa wa usalama inaibua maswali kuhusu uwezekano wa serikali kuhusika na ghasia hizo
“Huwezi kuwatishia wakenya kwa njia hiyo ili kujinusuru kisiasa; madhara yake ni makubwa. Wakati Wakenya wataanza kupinga vitendo hivi, hutaweza tena kuidhibiti nchi.” Matiang’i amesema.
Aidha ameishutumu serikali kwa kile alichokitaja kuwa “ugaidi wa kidijitali” udhibiti wa mitandao ya kijamii, propaganda na kukatiza huduma za mawasiliano kuwalenga viongozi wa upinzani.
Amesema hatua hizo, anazodai zinafanywa na serikali, zinaweza kudhoofisha taasisi huru na kuhatarisha utulivu wa nchi.
“Wameanzisha wimbi jipya la uchunguzi wa mawasiliano kidijitali dhidi ya upinzani. Tunafuatiliwa na magari ambayo ninaamini ni ya serikali.” Ameongeza.
Wakati uo huo amedai kuwa baadhi ya taasisi za serikali na vyombo vya usalama viko chini ya shinikizo la kisiasa, akisema hali hiyo inaathiri uhuru wao wa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Amesema serikali haifai kuweka maslahi ya kisiasa mbele ya uhuru wa taasisi za umma na vyombo vya usalama, akionya kuwa kufanya hivyo kunaweza kudhoofisha misingi ya utawala na imani ya wananchi katika taasisi hizo.
“Maslahi ya kisiasa hayafai kuwekwa mbele ya uhuru wa taasisi za umma na vyombo vya usalama, kwa kuwa kufanya hivyo kunadhoofisha uwezo wao wa kutekeleza majukumu yao na kupunguza imani ya wananchi.” Matiang’i ameeleza.
Matiang’i pia ametoa wito kwa viongozi wa upinzani kudumisha umoja licha ya shinikizo la kisiasa na juhudi za kuwagawanya.
Ameonya viongozi hao dhidi ya kuruhusu tofauti zao za kisiasa kudhoofisha umoja wao akisema upinzani unapaswa kuendelea kuzungumzia masuala yanayowahusu Wakenya.
Wakati uo huo Matiang’i ameeleza wasiwasi wake kuhusu kile anachodai kuwa ni kuingiliwa kwa vyombo vya usalama kwa maslahi ya kisiasa akisema hali hiyo inaweza kuathiri utendakazi wa maafisa wa usalama na kudhoofisha uwezo wao wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na bila upendeleo.









