Mshirika wa Karibu wa Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Irungu Nyakera amejiondoa rasmi katika kinyanganyiro cha Ugavana wa Nairobi na sasa analenga kuwania Ubunge wa Makadara katika uchaguzi mkuu ujao.
Nyakera ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Wizara ya uchukuzi amesema amefanya uamuzi huo kufuatia mashauriano ya kina na Kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua Pamoja na kusikiliza matakwa ya wakazi wa Makadara waliomtaka kuwania nafasi hiyo.
Nyakera amesema wakazi hao wamemwomba arudi nyumbani na ajitolee kuwawakilisha bungeni, jambo analosema limechangia kwa kiasi kikubwa kubadili mwelekeo wa kisiasa.
“Baada ya kushauriana na washauri wangu wa kisiasa, na muhimu zaidi, baada ya kuwasikiliza wananchi wa Makadara ambao wamenitaka nirejee nyumbani na kujitolea kuwa Mbunge wao, nimeamua kubadili mwelekeo wangu wa kisiasa kutoka kwa kinyang’anyiro cha ugavana wa Nairobi na kuelekeza nguvu zangu katika kuwania ubunge wa Makadara,” Nyakera amesema.
Kabla ya Kutangaza uamuzi huo Nyakera alisafiri hadi Wamunyoro, Kaunti ya Nyeri akiandamana na ujumbe wa wakazi wa Makadara na kukutana na Gachagua katika makazi yake.
“Mimi, pamoja na ujumbe kutoka Makadara, nilimtembelea Mheshimiwa Rigathi Gachagua nyumbani kwake Wamunyoro. Ninamshukuru kwa kuwa mshauri wangu wa kisiasa, kwa mwongozo na ushauri wake, na kwa kutupokea kwa uchangamfu,” Nyakera amesema.
“Ninashukuru sana kwa baraka zake ninapoanza safari hii mpya ya kuwa Mbunge ajaye wa Makadara chini ya Chama cha DCP.” Ameongeza.
Ubunge wa Makadara kwa sasa unashikiliwa na George Aladwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa ODM Tawi la Nairobi.
Aladwa tayari ametangaza nia ya Kuwania Ugavana wa Nairobi hivyo kuwacha nafasi ya Ubunge wa Makadara ukiwa wazi.









