Juhudi za baadhi ya wanasiasa kutoka Pwani kutaka kubuni chama chao cha kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 zimeibua mkinzano mkali katika chama cha ODM huku kiongozi wa chama hicho Raila Odinga akitofautiana wazi na gavana wa Kilifi Amason Kingi.
Licha ya Kingi kumtaka Odinga kukoma kulizungumzia suala hilo kwenye misururu ya mikutano yake ya kisiasa eneo la Pwani, Odinga amemtaka gavana huyo kusalia ODM kwani ndicho kimemfaidi hadi akawa Gavana.
Kwa upande wake Kingi ametetea shinikizo lake la eneo hilo kuwa na chama chao cha kisiasa ili kuwaleta pamoja viongozi wote wa Pwani na kuwa na usemi katika siasa za kitaifa.
Odinga vile vile ameendelea kunadi mema anayosema yako kwenye mswada wa BBI akisema yatakuwa na manufaa kwa Wakenya wote wakiwemo wananchi wa Pwani.
Wakati uo huo, Odinga amesema anaunga mkono hatua ya Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho kutafuta tiketi ya kuwania Urais kupitia kwa chama hicho.
Odinga amesema kila mwanachama wa Chungwa ikiwemo Joho ambaye ni naibu wake katika chama hicho, ana haki ya kushiriki mchujo wa kutafuta atakayepeperusha bendera yao kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Waziri huyo mkuu wa zamani amesalia kimya kuhusiana na iwapo atawasilisha stakabadhi zake kutaka kuwania tena Urais kupitia kwa chama hicho.