Uchaguzi wa Useneta katika kaunti ya Garissa sawa na chaguzi ndogo za ubunge katika maeneo ya Juja na Bonchari utaandaliwa Mei, 18 mwaka huu.
Tangazo hili limetolewa na tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC ambayo kupitia kwa mwenyekiti wake Wafula Chebukati imewataka wanaokusudia kushiriki kwenye chaguzi hizo kutuma stakabadhi zao kufikia Machi 8.
Aidha, vyama vya kisiasa vimepewa hadi Machi 22 kuwasilisha majina ya wawaniaji wake watakaoshiriki kwenye chaguzi hizo.
Kampeini za kujipigia debe zinatarajiwa kuanza Machi 29 na kukamilika Mei 15.
Kiti cha Useneta Garissa kilisalia wazi kufuatia kifo cha Yusuf Hajji Febuari 15 baada ya kuugua kwa muda mrefu huku maeneo bunge ya Bonchari na Juja yakisalia wazi kufuatia vifo vya Oroo Oyioka na Francis Waititu mtawalio.