Wanaume wawili wamehukumiwa kifungo cha miaka 28 gerezani baada ya kushtakiwa na makosa ya kumnajisi msichana wa miaka 16 huko lkaunti yan Kilifi.
Akitoa uamuzi huo, hakimu Charles Obulutsa amesema upande wa mashtaka umewasilisha Ushahidi wa kutosha kuidhinisha wawili hao walihusika na kitendo hicho.
“Mahakama hii imeridhishwa na ushahidi ambao upande wa mashtaka umewasilisha na hivyo kuwapata wawili na hatia”, hakimu Obulutsa amesema.
Wawili hao ambao ni Gift Kalu Mwango wa miaka 21 na Emmanuel Kazungu Mganga wa miaka 19 ambao walikuwa ni majirani ya mwadhiriwa, wanaripotiwa kumvamia akiwa ametoka nje kuchukua viatu mwendo wa saa nne usiku mnamo tarehe tisa mwezi Februari mwaka jana.
Baada ya kumvamia, wawili hao wanaarifiwa kumsukuma msichana huyo kichakani ambapo Mwango alimnajisi huku Mganga akimtishia kwa kisu.
Licha ya Mganga kutoshiriki katika kumnajisi msichana huyo, mahakama imempata na hatia ya kutazama kitendo hicho ilhali alikuwa na nafasi ya kukikomesha au kuondoka kutoka sehemu ya tukio.









