Bunge la kitaifa limewasilisha mahakamani majibu kuhusu kesi inayopinga mchakato wa kuwapiga msasa Mwenyekiti na Makamishna wateule wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Kupitia majibu yake, Bunge linadai kuwa kesi hiyo imewasilishwa mapema kabla ya wakati mwafaka, ikizingatia kuwa mchakato huo bado unaendelea ndani ya Bungeni.
Bunge limeeleza kuwa ombi hilo, lililowasilishwa na Kelvin Roy Omondi na Boniface Mwangi, ni la kubahatisha na halina msingi wa kisheria kwa kuwa linakiuka kanuni ya ukamilifu wa jambo.
Katika majibu hayo, Bunge limeongeza kuwa walalamishi hawajatumia kikamilifu njia zote zilizopo kikatiba kabla ya kukimbilia mahakamani, hivyo basi, kesi hiyo ni ya mapema na haijakomaa.
Kisheria, baada ya Rais kuwasilisha ujumbe kuhusu uteuzi wa Mwenyekiti na Makamishna wa IEBC, Spika wa Bunge huwasilisha ujumbe huo kwa Bunge na kuupeleka kwa Kamati ya Haki na Masuala ya Sheria kwa ajili ya mchujo.
Baada ya mchakato huo, unaojumuisha ushirikishwaji wa umma, kamati hiyo huwasilisha Ripoti Bungeni kwa mjadala na kupigiwa kura ya kuidhinisha au kukataa majina hayo.
Bunge linaeleza kuwa walalamishi walipaswa kwanza kuwasilisha malalamiko yao kwa Bunge kabla ya kuenda mahakamani.
“Katiba inalitunuku Bunge la Taifa mamlaka ya kuidhinisha uteuzi wa watu wanaopendekezwa kwa nyadhifa za tume huru na ofisi huru kama sehemu ya mizania ya madaraka baina ya mihimili ya serikali,” limeeleza Bunge katika kiapo chake.
Aidha, limeongeza: “Maslahi ya umma yanaunga mkono kwa kiasi kikubwa kuendelezwa kwa mchakato huu wa kuidhinisha uteuzi, hasa ikizingatiwa kuwa wananchi tayari wamewasilisha maoni yao na wanatarajia yatashughulikiwa na Kamati.”
Bunge sasa limeiomba Mahakama Kuu kufutilia mbali uamuzi wa tarehe 13 Mei kusitisha mchakato huo wa kuwapiga msasa waliotuliwa hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa kikamilifu.
Jaji Justice Lawrence Mugambi, anatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu kesi hiyo tarehe 29 Mei.










