Sehemu ya Kanisa la Jesus Is Alive Ministries linaloongozwa na aliyekuwa mbunge wa Starehe Askofu Margret Wanjiru limebomolewa alasiri hii.
Kulingana na Askofu Wanjiru, ubomozi huo umetekelezwa na watu waliodai kutumwa na Shirika la Reli la Kenya linalodai umiliki wa sehemu ya shamba la kanisa hilo.
Askofu Wanjiru amedokeza kuwa ubomozi huo na maafisa wa Polisi kutoka idara ya Ujasusi NIS na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI waliomnyanganya simu yake na kumjeruhi.
“Kuna Mungu Mbinguni. Ikiwa serikali ya Kenya Kwanza inaweza kuthubutu kugusa mali yangu, vipi kuhusu raia wasiojiweza?” Wanjiru alihoji.
“Tutaenda wapi ikiwa serikali yetu inatukandamiza? Tutakimbilia wapi? ’’
Wanjiru amedai kuwa kuna baadhi ya wakuu wa serikali ya kenya kwanza wanaoskuma kanisa lake kubomolewa licha ya kwamba alikempenia utawala wa sasa kuchaguliwa.
“Siamini walichonitendea. Ni mimi nilikua mstari wa mbele kuuza sera ya UDA. Ni mimi niliwapea jukwaa. Ni mimi niliwapa ruwaza ya Nairobi.’’
Pamekuwa na vuta nikuvute kati ya shirika la kenya railways na makanisa ya Askofu Wanjiru na Kanisa la Neno evangelism la Apostle James Nganga kuhusu umiliki wa mashamba ambayo makanisa hayo yamejengwa katikati mwa jiji la Nairobi.









