Mtihani wa kitaifa wa darasa la nane wa KCPE umengoa nanga kote nchini hii leo huku watahiniwa million moja, elfu mia moja themanini na saba, mia tano na kumi na saba wakikalia mtihani huo.
Akizungumza mjini Thika, kaunti ya Kiambu, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha amesema wameweka mikakati yote ya kuzuia visa vya udanganyifu.
Mwenyekiti wa baraza la mitihani nchini KNEC John Onsati naye yuko katika kaunti ya Mombasa ambapo ameshuhudiwa usmabazaji wa karatasi za mtihani katika shule mbalimbali eneo hilo.
Naye afisa mkuu mtendaji wa tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC Nancy Macharia amekuwa katika kaunti ya Kisumu ambapo amewataka walimu wakuu kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi amekalia mtihani huo.
Asubuhi ya leo, watahiniwa hao wamekalia somo la hisabati likifuatwa na somo la Kiingereza, kabla ya kumaliza siku na insha ya Kiingereza.
Hapo kesho, watahiniwa hao wa darasa la nane watakalia somo la Sayansi, Kiswahili Lugha na Kiswahili Insha kabla ya kumaliza mtihani wao siku ya Alhamisi na somo la kijamii na dini.
Hii ni mara ya kwanza kwa mtihani wa kitaifa wa KCPE kufanyika mwezi wa tatu badala ya mwezi wa Novemba ilivyo desturi.
Hii ni kutokana na janga la covid19 ambalo liliathiri kalenda ya masomo, huku shule zikifungwa kwa miezi tisa mwaka uliopita.