Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru anakabiliwa na tishio la kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kuhusiana na sakata ya shilingi million 23.
Katika taarifa Afisa mkuu mtendaji wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC Twalib Mbarak anasema wanachunguza madai kuwa Gavana huyo na maafisa wengine wa kaunti walilipwa pesa hizo kama marupurupu ya safari ambazo hazikufanyika.
Makachero wa EACC wamevamia makaazi ya Gavana huyo mapema hii leo kutafuta stakabadhi za kubaini iwapo pesa hizo ziliporwa.
Makachero hao walifika nyumbani kwa Waiguru kijijini Kagio kaunti ya Kirinyaga mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi, kutafuta ushahidi wa madai ya ufisadi na utumizi mbaya wa afisi yaliyoibuliwa na waakilishi wadi kwenye hoja ya kumngatua madarakani.
Makachero hao pia wamevamia makaazi ya Gavana huyo katika kaunti ya Nairobi na pia afisi zake huku makaazi ya maafisa wengine wa kaunti hiyo pia yakivamiwa.
Mwezi uliopita, maafisa wa EACC walimhoji Waiguru kwa muda wa takribani saa nane baada ya kamati ya bunge la seneti kupendekeza kuchunguzwa kwa Gavana huyo kubaini iwapo amefyonza mali ya umma.
Hata hivyo kamati hiyo ya fedha na uhasibu ilitupilia mbali hoja ya kumbandua Waiguru madarakani na kusema hakukuwa na ushahidi wa kuonyesha alihusika moja kwa moja na madai yaliyotolewa na waakilishi wadi hao.









