Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) imeorodhesha wagombea tisa watakaofanyiwa usaili kwa wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji (CEO).
Katika taarifa yake, IEBC imesema ilipokea jumla ya maombi 304 baada ya kutangaza nafasi hiyo wazi Julai 28, 2026.
Kipindi cha kutuma maombi kilifungwa Agosti 11, mwaka 2026.
“Orodha ya mwisho ya wagombea ilizingatia haja ya kuimarisha ujumuishaji, hususan uwiano wa kijinsia, uwakilishi wa kikanda na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu.” Tume hiyo imesema,
Walioorodheshwa ni Kaimu Mkurugenzi katika Mamlaka ya Kukabili matumizi ya pombe na dawa za kulevya (NACADA) Anthony Omerikwa kutoka Kaunti ya Busia, aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) Halakhe Waqo kutoka Marsabit, Harley Mutisya kutoka Makueni, Edmund Odiwuor Malitt kutoka Homa Bay na Andrew Gitau Kimani kutoka Nairobi.
Wengine ni Mohamed Abdullahi Abdi kutoka Kaunti ya Wajir, Edward Katama Ngeywa kutoka Trans Nzoia, Martina Wato Yattani kutoka Marsabit na Nelly Ilongo kutoka Taita Taveta.
Usaili huo umepangwa kufanyika Novemba 12 na 13, 2026. Kila mgombea akitarajiwa kuarifiwa binafsi kuhusu ukumbi atakaofanyiwa mchujo.
“Tume imewasiliana na kila mgombea binafsi kumfahamisha ukumbi atakaofanyiwa usaili.” IEBC imesema,
Wadhifa huo uliachwa wazi kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Hussein Marjan Hussein.








