Serikali imeagiza wizara zote, idara, taasisi na asasi za umma kupunguza matumizi ya fedha maramoja.
Kupitia kwa taarifa, mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei ameagiza taasisi zote za serikali kuanisha matumizi yake ya fedha kulingana na mwongozo wa wizara ya hazina ya kitaifa.
Kufuatia tangazo hilo, ina maana kwamba uagizaji na ununuzi wa mavazi yaliyo na nembo za taasisi za umma umesitishwa ikiwa ni pamoja na vitabu, mivuli, kalamu, vikombe na kalenda.
Haya yanajiri siku moja baada ya Rais William Ruto kuwaagiza maafisa wakuu watendaji wa taasisi za umma kupunguza bajeti zao kwa asilimia 30 pamoja na kuashiria kufungwa kwa taasisi ambazo hazitengenezi faida yoyote.
Katika mkutano na wakuu wa mashirika ya serikali na maafisa wakuu watendaji wa taasisi mbalimbali za umaa kwenye Ikulu ya Nairobi Rais alisema wakuu wa mashirika ya serikali na maafisa wakuu watendaji wa taasisi mbalimbali za umaa.
“Taasisi hizi ambazo hazitengenezi faida na hazina mipango yoyote au nia ya kufanya lolote kuhusu hilo zinafaa kufungwa na wafanyikazi wake kuhudumu kwingine. Na baadhi ya taasisi hizo zinafaa kujitolea kufungwa ili kuia wakenya wawache kupoteza pesa zao,” Rais alisema.
Mkutano huo pia uliangazia mpango wa kupunguza bajeti ya taaasisi hizo na kubinafsishwa kwa mashirika mbalimbali ya umma kufuatia kiongozi wa taifa kutia saini marekebisho ya sharia ya ubinafsishaji Novemba mwaka jana, hatua ambayo inatarajiwa kurahisha zoezi la kubinafsisha kampuni zinazomilikiwa na serikali.
Hatua ya kubinafsishwa kwa kampuni hizo ulipata pingamizi kutoka kwa wakenya na viongozi wa upinzani hofu ukizuliwa kuwa huenda mchakato huo ukatumiwa kufaidi watu wenye ukaribu na wakuu wa utawala wa Rais Ruto.